Balozi Matinyi awasilisha hati za utambulisho kwa mfalme wa Sweden

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 03:28 PM Jun 14 2025
Balozi Matinyi awasilisha hati za utambulisho kwa mfalme wa Sweden
PICHA: HALFAN CHUSI
Balozi Matinyi awasilisha hati za utambulisho kwa mfalme wa Sweden

BALOZI wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, amewasilisha rasmi Hati za Utambulisho kwa Mfalme wa nchi hiyo Carl XVI Gustaf, katika hafla maalum iliyofanyika katika Kasri la Mfalme wa nchini huko jijini Stockholm.

Baada ya mazungumzo mafupi kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufalme wa Uswidi, Matinyi alisindikizwa kwa gwaride rasmi kuelekea kwenye Kasri la Kifalme na kuwasilisha hati hizo kwa Mfalme Gustaf, ikiwa ni ishara rasmi ya kuanza kazi yake kama mwakilishi wa Tanzania nchini Sweden.

Katika mazungumzo yao Matinyi amemfikishia Mfalme huyo salamu binafsi za Rais Samia Suluhu Hassan, serikali na watu wa Uswidi.

Matinyi amemwelezea Mfalme huyo dhamira ya Tanzania ya kuendeleza na kuimarisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo baina ya nchi hizo na nia ya kukuza ushirikiano katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, hususani katika uwekezaji, biashara, utalii, elimu na mafunzo ya ufundi, afya, nishati, miundombinu, utunzaji mazingira, pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

Kwa upande wake, Mfalme  Gustaf ametuma salamu za undugu na urafiki kwa Rais Samia na kueleza kuwa nchi yake ya Uswidi itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa manufaa ya mataifa yote mawili, hususani katika kuendeleza sekta za viwanda, nishati, madini, utalii na elimu.

Itakumbukwa kuwa, Balozi Matinyi aliteuliwa na Rais  Samia kuwa Balozi wa Tanzania nchini humo Machi  25 mwaka huu, sambamba na jukumu jilo pia ana jukumu la kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Denmark, Finland, Iceland, Norway, Estonia, Latvia, Lithuania Ukraine, Stockholm.