Serikali kujenga chumba kunusuru vichanga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:42 PM Jun 13 2025
Serikali kujenga chumba kunusuru vichanga
PICHA: MTANDAO
Serikali kujenga chumba kunusuru vichanga

SERIKALI imetoa Shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa chumba maalum cha uangalizi watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa na uzito pungufu na changamoto ya upumuaji ili kunusuru maisha yao.

Vilevile, serikali imesema itaweka vifaa maalum katika vituo 100 vya afya nchini kwa ajili ya kukabiliana na matatizo hayo yanayowakabili watoto hao baada ya kuzaliwa. Hayo yalisemwa juzi na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama wakati akipokea taulo za watoto kutoka Kampuni ya Sunda zaidi ya kasha 1,600 zenye thamani ya Shilingi milioni 65.

Jenista, alisema lengo la serikali ni kuhakikisha watoto wanahudumiwa kwa dharura kwa kutengenezewa mahali maalum katika vituo vya afya nchini ili kuokoa maisha yao. Alisema vituo hivyo, pia vitawekewa vifaa vya kusaidia wa watoto kusikia na tiba.

"Mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan amevunja rekodi kwa kufanya vizuri kwenye malengo ya maendeleo endelevu, lengo namba tatu kwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano na vya wajawazito wakati wa kujifungua , " alisema.

 Alisema Samia amesaidia kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kutoka 556 kati ya vizazi hai 100,000 hadi kufikia 104 kwa kuboresha huduma ya mama na upasuaji wa dharura. Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Andy Liu, alisema wametoa msaada huo kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha huduma bora kwa watoto. 

Mkuu wa Mkoa huo, Rosemary Senyamule, alisema msaada huo ni muhimu kwa wanawake wa Dodoma kuboresha huduma za afya. Senyamule, alisema kwa kipindi cha miaka minne, zaidi ya Shilingi bilioni 80 zimetumika kuboresha huduma za afya na miundombinu mkoani Dodoma.

Alisema kati ya hizo, Shilingi bilioni 42.13 zilitumika kwenye miundombinu na bilioni 38 vifaa tiba na vitendanishi. Alisema hadi sasa halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma zina hospitali.