Wachimbaji wavamia mapori kusaka madini

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 03:20 PM Jun 13 2025
Madini
PICHA: MTANDAO
Madini

MAPORI ya akiba ya Rungwa, Kizigo na Muhesi yaliyopo wilayani hapa Mkoa wa Singida yanadaiwa kuvamiwa na wachimbaji wadogo wa madini na kuanza uchimbaji bila ya kuwa na kibali.

Hayo yamebainika juzi wakati ziara ya  Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa huo ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani hapa. Kamati hiyo iliongozwa na  Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo, Martha Mlata na Mkuu wa Mkoa, Halima Dendego.

Akizungumza katika ziara hiyo,  Dendego, alisema kuna taarifa za uwepo wa madini katika mapori hayo  kunufaisha watu wachache baada ya kuvamia na kufanya shughuli za uchimbaji bila kibali. “Maeneo hayo yamekuwa na madini na vijana wanavamia pasipo mpangilio, tufanye utafiti kubaini maeneo hayo, tuombe kibali kwa mamlaka husika wananchi na vijana wetu waweze kupata leseni ili wachimbe kwa kufata utaratibu na hii itakuza mapato kwao na  pia halmashauri husika," alisema.

 Dendego katika kuhakikisha suala linafanyiwa kazi haraka, aliunda kamati ya wajumbe maalum ya kufanya utafiti wa kina juu ya uwepo wa madini hayo katika mapori hayo na kutambua mipaka ya eneo hilo. Alisema Mhifadhi wa Mapori na Waziri wa Maliasili na Utalii, wameridhia ufanyike utaratibu wa kutambua maeneo yenye madini mkoani humo ili kuombewa kibali na leseni kwa wachimbaji kufanya shughuli zao.

Mlata, akizungumzia suala hilo, alisema mkoa unakwenda kupata  maendeleo ya kasi kutokana na uwepo wa madini katika wilaya hiyo. Alishauri leseni zilizopo zifutwe ili baada ya utafiti, wanufaika wa kwanza wa madini hayo wawe wakazi wa Singida na halmashauri zake.