Maaskofu 500 wa Kanisa Gwajima watinga Mahakama Kuu

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 03:14 PM Jun 13 2025
Maaskofu
Picha: Mpigapicha Wetu
Maaskofu

Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church maarufu kama Kanisa la Ufufuo na Uzima, limefungua kesi Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma likiomba amri ya muda ya kuondoa zuio lililowekwa na serikali dhidi ya kuendelea kwa shughuli zake za kidini huku maaskofu takribani 500 wakifika kusikiliza kesi hiyo.

WKesi hiyo inalenga kulinda hadhi ya usajili wa kanisa hilo huku rufaa dhidi ya zuio hilo ikiendelea kusikilizwa.

Kanisa hilo linaongozwa na Askofu Josephat Gwajima ambaye pia ni Mbunge wa Kawe kwa chama cha Mapinduzi (CCM).

Hivi karibuni mamlaka za serikali zilifunga kanisa hilo kwa madai kwamba linaendesha shughuli kinyume na masharti ya leseni ya usajili wake.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mamlaka baadhi ya shughuli zinazaofanyika ndani ya kanisa hilo zimeelezwa kuwa ni za kisiasa kupita kiasi na hazilingani na malengo ya asili ya taasisi hiyo kama ilivyosajiliwa.

1

Wakili wa Kanisa hilo Peter Kibatala, amesema kanisa hilo limewasilisha shauri namba 13189 la mwaka 2025 dhidi ya mkuu wa Jehi la polisi (IGP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msajili wa taasisi za kiraia.

Katika shauri hilo kanisa hilo linaomba mahakama kutoa amri ya muda itakayoruhusu kuendelea kwa ibada na shughuli nyingine za kidini hadi pale rufaa iliyowasilishwa kupinga hatua ya serikali kufungia kanisa hilo itakaposikilizwa na kuamuliwa rasmi.