Wakili Majaliwa ageukia Ubunge Kigamboni, urais wamshinda

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:55 AM Jun 13 2025

Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Majaliwa
Picha: Mpigapicha Wetu
Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Majaliwa

Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Majaliwa aliyetangaza kugombea urais ageukia Ubunge Jimbo la Kigamboni ni baada ya chama chake cha National Reconstruction Alliance (NRA) kumpa nafasi ya kujifunza zaidi ndani ya Bunge la Jamhuri la Muungano Tanzania.

Aidha, Wakili Majaliwa amesema hana fedha za kwenda kutapanya na kugawa kwa watu ili wamchague, muda utakapofika wakuanza kampeni kwa ruhusa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ataweka hadharani kwa nini ana omba ridhaa hiyo.

Wakili Majaliwa amesema haya leo Juni 13,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dar es Salaam kwamba wiki chache zilizopita alitangaza jina lake kuingiza kwenye kinyang'anyiro cha nafasi ya urais kupitia chama chake.

"Jina langu kwa mujibu wa Kanuni na Katiba za Chama lilingia katika mchujo na mwisho siku Mkutano Mkuu wa Chama uliazimia kunipa nafasi nyingine ya kupata uzoefu na ujuzi mwingine zaidi katika masuala ya chaguzi za kisiasa,"

"Kwa ajili hiyo uongozi wa juu wa chama na vikao vyake ulinipa maelekezo kuelekeza nguvu katika Bunge ambako ndiyo chombo maalum katika utatuzi wa kero za wananchi, rasmi natangaza kwamba ninaazimia kwenda kusimamisha jina langu kugombea Ubunge katika Jimbo la Kigamboni," amesema Wakili Majaliwa 

Amesema huo ni ujumbe kwa wana Kigamboni wote na vitongoji vyake na kata zake zote tisa zinazounda jimbo kubwa la Kigamboni, kwamba anakwenda huko anaomba wampokee kama kijana wao.

"Mimi ni mtoto wenu na mdogo wenu mnipokee nina kuja kama mtanzania wa kawaida kabisa mwenye kipato cha kawaida nisiye na vishindo wala mikogo nisiyekuwa na wapambe wala vihelele wala machawa nakuja nikiwa na silaha zangu muhimu kichwani,"

"Mwezi Oktoba kwa mujibu wa Katiba ndiyo mwezi wa uchaguzi tunakwenda kufanya uchaguzi kupata rais, wabunge na madiwani. Nitumie nafasi hii kuliombea Taifa uchaguzi huu ukawe wa amani na mshindi akapatinae kwa kufuata Katiba, Sheria na taratibu bila kumdhulu  mtu yeyote," amesema Wakili Majaliwa