NIRC kuchimba visima 67,000

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 02:23 PM Jun 13 2025
Uchimbaji visima
PICHA: RENATHA MSUNGU
Uchimbaji visima

TUME ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imeanza kutekeleza ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuchimba visima virefu 67,000 kwa ajili ya kuinua kilimo cha umwagiliaji nchini na taifa kukabiliana na uhaba wa chakula.

Ahadi hiyo ilitolewa na Samia wakati wa kilelel cha  Maadhimisho ya Siku ya Wakulima Duniani maarufu kama Nanenane iliyofanyika kitaifa Nyanda za Juu Kusini mkoani Mbeya mwaka juzi. Hayo yalisemwa jana jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa, wakati wa kuanza uchimbaji wa visima hivyo kwa kutumia mitambo iliyonunuliwa na Serikali katika shamba la Chinangali ambalo ni miongoni mwa programu ya  Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kuwawezesha vijana kujiajiri katika kilimo.

Mndolwa, alisema Serikali imeiwezesha tume hiyo kununua mitambo ya kisasa ya kuchimba visima hiyo ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi ya upatikanaji wa maji kwa kiliimo cha umwagiliaji na Taifa kuondokana na kilimo cha msimu mmoja wa mvua na kulima zaidi ya mara mbili. “Tume imenunua mitambo 17 ya kuchimba visima kwa thamani ya shilingi bilioni 17.5 yenye uwezo wa kuchimba mita 300 hadi 1,800, “ alisema na kuongeza kuwa:

 â€œMitambo saba inachimba visima katika shamba hili la Chinangali na tunashuhudia visima vikiwa na maji ya kutosha kabisa. " Alisema miundombinu ya umwagiliaji katika shamba hilo imekamilika na kinachofuata ni kuhakikisha maji yanapatikana kwa kuchimba visima 29 hapo na vingine 40 shamba la BBT la Ndogowe ili vijana walime kwa uhakika.  Mndolwa, alisema, dhamira hiyo haishii Chinangali na Ndogowe, bali itaendelea kwa nchi nzima ili kuhakikisha wakulima wanaendelesha kilimo endelevu na nchi kupata chakula cha kutosha.

 "Mitambo hii itapita mkoa kwa mkoa, wakulima wajiandae kuchangamkia fursa hii wakiwa katika makundi ya zaidi ya 16 na ekari kuanzia 40 ili waweze kupata kisima," alisema. Alisema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Samia, miradi ya umwagiliaji imeongezeka kutoka 13 hadi kufikia 780.