Dk.Kijaji azindua mnada wa mpakani

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 02:43 PM May 28 2025
Dk.Kijaji azindua mnada wa mpakani
PICHA: MTANDAO
Dk.Kijaji azindua mnada wa mpakani

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji amezindua mnada wa Mpakani Kileo uliopo wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro ambao unatarajiwa utaongeza masoko ya mifugo.

Mnada huo ambao utakuwa fursa ya kimkakati kuyafikia masoko ya ndani na nje ya nchi una uzio wa mzunguko wa mita 500, kipakilio, mazizi, choo pamoja na miundombinu ya maji kwa ajili ya wafugaji na wafanyabiashara Mkoani Kilimanjaro umegharimu Sh.milioni  208.924 hadi kukamilika.

“Mnada huu una uwezo wa kupokea ng’ombe 500 na mbuzi na kondoo 3000 kwa mara moja na hivyo ni imani yangu kuwa uwekezaji huu utaleta tija na miundombinu iliyojengwa itatunzwa na kulindwa," alisema Dk. Kijaji.

Alisema ujenzi wa mnada huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa dhamira njema ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa wafugaji na wadau wa mifugo nchini katika kupanua masoko ya mifugo ndani na nje ya nchi. Alisema hadi sasa minada ya mifugo 51 yenye thamani ya Sh. Bilioni 17.5 imejengwa na kukarabatiwa hapa nchini ambayo imewezesha ongezeko la biashara ya mifugo nchini.

Dk.Kijaji kutokana na uwepo wa minada, mifugo iliyouzwa katika minada hiyo imeongezeka kutoka Sh. Trilioni 1.5 2021/22 hadi kufikia Sh. Trilioni 3.7 mwaka 2024/25. Aidha, Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi amewataka wafanyabiashara ya mifugo hususani wanaosafirisha mifugo kwenda nje ya nchi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi katika kufanya biashara hiyo.

Aliongeza kuwa kumekuwepo na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao kwa makusudi hufanya biashara kinyume na taratibu, na hutumika na wafanyabiashara wa nchi jirani kununua na kutorosha mifugo kwa siri kwa kutumia vipenyo visivyo rasmi kwenda nchi jirani.

Alisema wakati mwingine wafanyabiashara kutoka nchi jirani huingia na kwenda moja kwa moja katika minada ya awali kwa kuwatumia wenyeji kununua mifugo hiyo na kuisafirisha kinyume na taratibu kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Dk.Kijaji alisema kuwa  wanaofanya wanahujumu mapato ya Serikali na kudidimiza ustawi wa sekta ya mifugo nchini hivyo  serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi yao. Dk. Kijaji alisema watendaji wa Serikali ambao wanasimamia minada na vituo vya ukaguzi wa mifugo kutoa vibali vya biashara ya mifugo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ili kuepusha usumbufu kwa wafanyabiashara. 

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo),  Abdul Mhinte alisema mnada wa Mpakani wa Kileo ni moja ya mnada wa kimkakati kati ya minada 10 iliyopo mpakani mwa nchi, ikiwemo minada iliyopo Songea, Kagera, Tanga, Arusha na maeneo mengine yaliopo mpakani mwa nchi.

Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro,Kiseo Nzowa amesema wao kama Mkoa watahakikisha wanashirikiana na Halmashauri zote za Mkoa wa Kilimanjaro katika kuhakikisha miundombinu ya Mnada wa Mpakani Kileo inalindwa na kutunzwa ili iweze kutoa huduma na kutoa tija kwa wafugaji na wafanyabiashara wote wa Mifugo.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mwanahamisi Munkunda, alimshukuru Rais Dk.Samia na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dk.Kijaji kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya mnada wa Mpakani Kileo ambao utaongeza pato kwa wafugaji, wafanyabiashara na nchi kiujumla.