Wananchi Rufiji watakiwa kujiandaa fursa uwekezaji kilimo cha miwa na ndizi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 08:03 PM May 28 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Rufiji, Simon Berege.
Picha: Julieth Mkireri
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Rufiji, Simon Berege.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Rufiji, Simon Berege, amewataka wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kuanza kujiandaa kikamilifu ili kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazotokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea katika halmashauri hiyo, ukiwemo wa kilimo cha miwa na ndizi.

Akizungumza wakati wa Baraza la Biashara lililofanyika mjini Utete, Berege amesema miradi hiyo ya uwekezaji inalenga kuleta mageuzi ya kiuchumi katika Wilaya ya Rufiji, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua hatua mapema kwa kujipanga kiuwekezaji na kibiashara.

Ameeleza kuwa moja ya miradi mikubwa inayotekelezwa kwa sasa ni mradi wa kilimo cha miwa unaosimamiwa na Kampuni ya Lake Agro katika Kata ya Chemchem, pamoja na mradi wa kilimo cha ndizi unaoendeshwa na Kampuni ya Food Star Limited katika Kijiji cha Nyamwage, Kata ya Mbwara.

“Uwekezaji huu ni mkubwa na Rufiji inaenda kufunguka kiuchumi. Tunapaswa kuanza kufikiria kwa vitendo kuhusu namna tutakavyonufaika—kuanzia uanzishaji wa biashara mbalimbali hadi ujenzi wa nyumba za wageni, kwa kuwa idadi ya watu na wageni itaongezeka,” amesema Berege.

Berege ameongeza kuwa ni muhimu kwa wajasiriamali kuanza kufikiria namna ya kutoa huduma zinazohitajika na wawekezaji pamoja na wafanyakazi wao, ikiwa ni pamoja na mahitaji ya malazi, chakula, usafiri na bidhaa za matumizi ya kila siku.

“Hii ni fursa ya dhahabu kwa wananchi wa Rufiji. Tukiitumia vizuri, tunaweza kuinua hali ya maisha ya jamii yetu kwa kuongeza kipato na ajira,” amesisitiza.