Mbatia aibuka kidedea, mahakama yafuta uamuzi kumvua uanachama

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 07:27 PM May 28 2025
James Francis Mbatia.
Picha: Mtandao
James Francis Mbatia.

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Kuu Dar es Salaam, imetengua rasmi uamuzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi wa kumvua uanachama na kumwondoa James Francis Mbatia katika nafasi ya Uenyekiti wa Taifa wa chama hicho, ikieleza kuwa uamuzi huo ulikuwa batili kisheria.

Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji Abdi Kagomba, baada ya kupitia maombi ya mapitio yaliyowasilishwa na Mbatia dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya chama hicho.

“Uamuzi wa kumvua uanachama na kumuondoa katika nafasi ya uenyekiti mwombaji ulifanyika kinyume na kanuni, na alinyimwa haki ya kusikilizwa,” amesema Jaji Kagomba katika uamuzi wake.

Mahakama imebaini kuwa Mkutano Mkuu wa chama hicho, uliofanyika Septemba 24, 2022, ulimvua Mbatia uanachama na kumwondoa madarakani bila kumpa nafasi ya kujitetea, hatua ambayo ilikiuka misingi ya haki za asili.

“Uamuzi huo ulikiuka masharti ya Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 26(3)(o) ya Katiba ya NCCR-Mageuzi, pamoja na Kifungu cha 8(1) cha Sheria ya Vyama vya Siasa [Sura ya 258 R.E 2019],” ameeleza Jaji Kagomba.

Kutokana na ukiukwaji huo, Mahakama imefuta rasmi uamuzi wa Mkutano Mkuu wa NCCR-Mageuzi uliotolewa Septemba 24, 2022, ikisisitiza kuwa haukufuata utaratibu halali wa kikanuni.

Katika maombi yake, Mbatia amedai kuwa alivuliwa uanachama na nafasi ya Uenyekiti wa Taifa kwa njia isiyo halali, bila kuelezwa sababu wala kupewa fursa ya kujitetea, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Uamuzi huu umetolewa katika Mahakama Kuu jijini Dodoma, ukihitimisha mzozo wa muda mrefu uliokuwa ukilitikisa chama hicho kikongwe cha upinzani nchini.