Jumla ya migodi 13,279 pamoja na bohari za baruti 164 zimekaguliwa nchini kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025.
Hayo yameelezwa leo Mei 28, 2025 jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Idara ya Leseni wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Mhandisi Ramadhan Lwamo, katika kikao kazi cha wakaguzi wa migodi na baruti kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Amesema kuwa miongoni mwa migodi hiyo iliyokaguliwa ni migodi mikubwa saba, migodi ya kati 46, migodi midogo 13,226 pamoja na bohari za baruti 164.
“Kaguzi hizi zimeimarisha Sekta ya Madini na kuongeza makusanyo ya Serikali kupitia maduhuli, hivyo kuchangia katika kuimarisha uchumi na Pato la Taifa,” amesema Mhandisi Aziza.
Ameongeza kuwa, “Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ina matarajio makubwa kwa Sekta ya Madini kutokana na mchango wake mkubwa katika Pato la Taifa. Kufikia mwaka 2024, sekta hii ilichangia asilimia 10.1 ya Pato la Taifa, ikiwa ni zaidi ya lengo la asilimia 10 lililowekwa kufikiwa mwaka 2025.”
Mhandisi Aziza ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa ya Idara ya Ukaguzi wa Migodi, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha maduhuli ya Serikali katika sekta hiyo.
Aidha, amewakumbusha wakaguzi kuzingatia Sheria ya Madini Na. 123 katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu masuala ya afya na usalama mahali pa kazi, uhifadhi wa mazingira, na matumizi salama ya baruti ili kuepuka ajali.
“Naagiza kila mkoa kutambua maeneo yenye hatari kubwa ya ajali na kuyawasilisha kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi, ili kuweka mikakati shirikishi ya kuzuia ajali katika maeneo hayo,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema kikao hicho cha nne kwa wakaguzi wa migodi kinalenga kujengeana uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa kuwa wao ni uti wa mgongo wa usimamizi wa Sekta ya Madini.
“Wakaguzi wa migodi wana jukumu kubwa. Malengo ya ukusanyaji wa maduhuli yaliyowekwa na Serikali hutegemea vyanzo vya mapato vinavyosimamiwa na wakaguzi. Bila kulinda vyanzo hivyo, mapato hayawezi kupatikana. Tutaendelea kujifunza na kuboresha utendaji ili kuhakikisha tunafikia malengo,” amesema Mhandisi Kamando.
Aidha, amebainisha madhara ya kutofanya ukaguzi, yakiwemo ajali katika migodi zinazosababisha vifo, kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji, na kupungua kwa mapato ya Serikali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED