Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) imelaani vikali tabia ya baadhi ya vijana wa Kenya wanaotumia mitandao ya kijamii kumvunjia heshima Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mwenyekiti wa JMAT, Sheikh Dk. Alhad Mussa Salum, amesema Jumuiya hiyo imesikitishwa na matamshi ya kashfa na matusi yanayoendelea mitandaoni dhidi ya Rais Samia, wakiyahusisha na baadhi ya vijana wa nchi jirani ya Kenya.
“Sisi tunaamini Kenya ina viongozi wa dini, pamoja na viongozi wa serikali. Tunawaomba sana wazungumze na vijana wao na kuwasihi waache tabia ya kumvunjia heshima Rais wa nchi nyingine, ikiwemo Rais wa Tanzania,” amesema Sheikh Salum.
Sheikh huyo ameonya kuwa tabia ya matusi na dharau dhidi ya viongozi wa mataifa mengine siyo tu inavunja misingi ya heshima na uhusiano mzuri wa kidiplomasia, bali pia ni kosa mbele ya Mwenyezi Mungu.
“Tuwakumbushe kuwa heshima ya taifa lolote ni maadili ya watu wake. Ikiwa Wakenya wataendelea na matusi dhidi ya viongozi wa mataifa mengine, basi siyo tu watakuwa wanamkosea Mungu kwa kuwatusi wazazi wao, bali pia watakuwa wanapoteza ustaarabu wao mbele ya uso wa dunia,” ameongeza.
Sheikh Salum amesisitiza kuwa hali hiyo isipuuzwe kwani inaweza kusababisha mtafaruku wa kijamii na kidiplomasia iwapo haitazuiwa mapema.
“Tulipofika panatosha. Moto mkubwa huanza kama cheche ndogo, hivyo ipo haja ya kuzizima cheche hizi kabla hazijakuwa moto mkubwa,” amehitimisha.
JMAT imetoa wito kwa wananchi wote wa Afrika Mashariki kutumia mitandao ya kijamii kwa njia ya heshima, uadilifu na maadili, ili kulinda misingi ya amani na mshikamano katika ukanda huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED