No Reforms No Election yahamia Kaskazini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:19 PM May 27 2025
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, John Heche.
Picha: Mtandao
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, John Heche.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza rasmi uzinduzi wa Operesheni "No Reforms No Election" kwa Kanda ya Kaskazini, ikiwa ni sehemu ya msukumo wa kudai marekebisho ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Brenda Rupia, uzinduzi wa operesheni hiyo utafanyika kesho, Jumatano Mei 28, 2025, katika Uwanja wa Reli, jijini Arusha, kuanzia saa 7:00 mchana hadi saa 12:00 jioni.

Uzinduzi huo utaongozwa na viongozi waandamizi wa chama hicho akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, John Heche, na Katibu Mkuu wa chama, John Mnyika.

“Chama kinawahimiza wananchi wote wa Kanda ya Kaskazini – inayojumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara – pamoja na wanachama na wapenzi wa demokrasia, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hili muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Wakati huo huo, Kamati Kuu ya CHADEMA kupitia kikao chake kilichofanyika tarehe 23 na 24 Mei 2025, imemuidhinisha rasmi Ali Akalipo Juma kuwa Katibu wa Kanda ya Unguja – Zanzibar.

Taarifa ya uteuzi huo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za chama kuimarisha uongozi na utendaji katika ngazi ya kanda, hasa kuelekea kipindi muhimu cha kisiasa nchini.

Uzinduzi wa Operesheni No Reforms No Election umekuwa ukifanyika katika kanda mbalimbali nchini kama sehemu ya kampeni ya kudai mabadiliko ya sheria, mfumo wa uchaguzi huru na haki, na kuimarishwa kwa taasisi za kidemokrasia kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.