CHADEMA Zanzibar haina nia ya kususia Uchaguzi Mkuu 2025

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:26 PM May 27 2025
Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ali Ibrahim Juma.
Picha: Mtandao
Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ali Ibrahim Juma.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, kimesema hakina nia ya kususia uchaguzi mkuu 2025, bali kinataka mabadiliko ya mifumo wa uchaguzi ndio uchaguzi ufanyike kwa misingi ya haki kwa washiriki wote.

Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ali Ibrahim Juma, ameyasema hayo jana Visiwani Zanzibar wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa kamati maalum kwa masuala ya uendeshaji wa chama.

Amesema CHADEMA haina maana ya kususia uchaguzi mkuu lakini kufanya mabadiliko ya mifumo ili kuwe na usawa na haki kwa uchaguzi huru.

“Tunaamini kupitia mabadiliko tutawapa fursa wananchi kushiriki uchaguzi vizuri na matokeo yatangazwe kwa ukweli,”amesema.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo viongozi wa CHADEMA wa zamani na wapya ambao wamejaza nafasi kwa walioamua kuhama chama, na kwamba lengo ni kuwa na mipango na mikakati ya kukiinua chama.

Awali, Katibu Mkuu wa CHADEMA Taifa, John Mnyika amewataka Wanzanibari kuunga mkono kwa vitendo msimamo wa chama wa ‘No reforms No Election’ huku wakikumbuka kauli mbiu ya ndani ya chama ya  ‘Strong together’ imara pamoja)  na kuungana na wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini katika kupigania haki.

Amesema chama hicho bado ni imara na nguvu na kinaendelea na shughuli zake kama kawaida na kwamba nafasi zote za walioamua kutoka Ibara ya 6:35 imetumika kuziba nafasi za uongozi.

Amesema wameamua kukutana na viongozi wa visiwani humo kuwaeleza kwa kina kuhusu kauli mbiu ya CHADEMA ya ‘No Reforms No Election’.