Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kimemchagua Yusuph Wangira, kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho huku makamo akiwa ni Amana Selemani Mzee.
Katika uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika Wilaya ya Ubungo mkoa Dar es Salaam, wajumbe walikua ni 103 huku wagombea wakiwa watatu ambao ni Yusuf Wangira kura 52, Neema Nyerere kura 6 na Wilson Ellas kura 46.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi wa chama cha cha hicho jijini hapa Mwenyekiti wa uchaguzi huo Coaster Jimmy, amesema jumla ya wapigakura 103 na waliopigiwa kura walikuwa watatu, Neema Nyerere alipata kura 6 , Wilson Ellas 46 na Yusuph Wangira amepata kura 52 hivyo chama hicho kimemtangaza Yusuph Wangira ndiyo atakaye kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TLP.
Akishukuru wanachama katika uchaguzi huo Yusuph Wangira amesema anawahakikishia ushindi wa chama chao katika uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani mikoa yote na mgombea mweza wake Amana Selemani Mzee.
Kwa upande wake Msajili Msaidizi wa vyama vya Siasa Tanzania Sisty Nyahoza ,amewapongeza Tanzania Labour Party TLP, kwa kufanya uchaguzi kwa amani wa chama hicho .
Msajili Nyahoza amesema katika uchaguzi lazima ukubali mambo mawili kushinda na kushindwa na uchaguzi wenu umeenda vizuri demokrasia imefanya kazi hivyo aliwaomba wawe wamoja kama chama wafanye kazi za chama na kuwa wastamilivu aliwapongeza walioshinda na walishindwa.
Amesema vyama vitakavyoshiriki uchaguzi unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu ambapo kuna vyama 18 na vitashiriki uchaguzi na kuwataka wadumishe amani.
Kwa upande wake mgombea nafasi ya urais ndani ya Chama hicho, Wilson Ellas ambaye kura hazijatosha ameonesha kutoridhishwa kwa matokeo hayo ambapo amesema uchaguzi wa chama hicho siyo sahihi kwani amesema jumla ya wapiga kura ni 103 huku akidai kura zilikua 104 .
"Tulipata taarifa kuwa katika mkutano huo kumeingizwa mamluki, kura zimekua nyingi kuliko wapiga kura, hii sio haki, hapa hamna demokrasia ujanja ujanja umetumika, sikubaliani na matokeo"amesema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED