Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ambaye pia ni Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), ameiwakilisha serikali katika ibada maalum ya maziko ya Askofu Mkuu wa kwanza Mwafrika wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Hayati Dk. Immanuel Lazaro.
Askofu Dk. Immanuel (88), aliyefariki dunia Mei 17,2025 katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC, anazikwa leo katika Kanisa la Jerusalem-Mudio, Tarafa ya Masama, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
Hayati Askofu Dk. Immanuel, alianza kupata changamoto ya maradhi ya utu uzima tangu mwaka 2018 na alitibiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na baadae nchini India.
Baada ya mwaka mmoja wa afya yake kuonekana kuimarika, hali yake ilianza kudhoofu tena na alipata matibabu katika Hospitali ya Bugando-Mwanza, KCMC na Hospitali ya Safe ya Dar es Salaam.
Mei 15, 2025 alfajiri alizidiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu; na alifariki dunia Mei 17,2025 majira ya saa 5:40 asubuhi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED