Butondo akabidhi vifaa vya TEHAMA Shule za Sekondari Ngofila, Lagana

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:03 PM May 27 2025
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo (kushoto)akikabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Mkuu wa shule ya Sekondari Ngofila Matrida Mwaliaje.
Picha: Marco Maduhu
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo (kushoto)akikabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Mkuu wa shule ya Sekondari Ngofila Matrida Mwaliaje.

Mbunge wa Kishapu Boniphace Butondo, ameendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya wamu ya sita katika kuboresha sekta ya elimu hapa nchini, ambapo amekabidhi vifaa vya Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), kwa shule za Sekondari Ngofila na Lagana.

Amekabidhi vifaa hivyo jana katika shule hizo kwa nyakati tofauti, huku akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kishapu Shija Ntelezu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, amesema lengo lake  ni kuunga mkono Juhudi za Mheshimiwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, za kuboresha  sekta ya elimu, ili wanafunzi wasome kwa vitendo na kupata ufaulu mzuri.

“Vifaa vya TEHAMA ambavyo nimetoa ni Printer, Moniter Screen,CPU na Projector, vitakavyo saidia uinuaji wa taaluma kwa wanafunzi,”amesema Butondo.“Vifaa hivi vitawasaidia pia Walimu katika maandalizi ya masomo pamoja na kuchapa Mitihani,hakuna tena kwenda kwenye Stationary za watu binafsi, pia itapunguza na gharama za uaandaaji wa mitihani,”ameongeza.

Aidha, ametoa maelekezo kwamba,vifaa hivyo vitunzwe pamoja na kuzingatiwa usafi, sambamba na kuanzishwa masomo ya Computer hasa katika shule ya Lagana ambayo haina somo hilo.

Mkuu wa shule ya Sekondari Ngofila Matrida Mwaliaje, amesema vifaa hivyo vya TEHAMA ni chachu kubwa ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi, sababu watavitumia kuchapisha mitihani mara kwa mara kwa kuwapatia majaribio wanafunzi na kujua uwezo wao na kuongeza bidi zaidi za ufundishaji.

Amesema vifaa hivyo pia vimewaepusha na gharama kubwa ya kwenda kuchapisha mitihani katika shule kubwa ikiwamo ya Kishapu na Ukenyenge umbali wa kilomita 60, lakini sasa hivi watakuwa wakichapisha mitihani hapo hapo shuleni.

Naye Mkuu wa shule ya Sekondari Lagana Adam Malongo, ameshukuru kwa vifaa hivyo vya TEHAMA,kwamba ni msaada mkubwa kwa ustawi wa elimu.

Nao baadhi ya wanafunzi akiwamo Hadija Pambe, amesema vifaa hivyo ni msaada mkubwa katika masomo yao, sababu watakuwa wakisoma kwa vitendo na kupewa majaribio ya mitihani mara kwa mara.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kishapu Shija Ntelezu, amempongeza Mbunge Butondo kwa kuendelea kuunga mkono suala ya elimu, kwamba amekuwa akiitekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa Vitendo.

Aidha, Mbunge Butondo tayari ameshatoa vifaa vya TEHAMA katika Shule Tatu za Sekondari Jimboni humo, ikiwamo Kishapu Sekondari, Ngofila na Lagana.