JKT yatangaza nafasi za mafunzo kwa wahitimu Kidato cha Sita 2025

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 05:42 PM May 27 2025
Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Kanali Juma Mlay.
Picha: Renatha Msungu
Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Kanali Juma Mlay.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza rasmi nafasi za vijana waliohitimu kidato cha sita mwaka 2025 kutoka shule mbalimbali nchini, kujiunga na mafunzo ya kijeshi kwa mujibu wa sheria, kuanzia kesho Mei 28 hadi Juni 8, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Kanali Juma Mlay, amebainisha kuwa vijana walioteuliwa wanapaswa kuangalia majina yao pamoja na kambi walizopangiwa kupitia tovuti rasmi ya Jeshi la Kujenga Taifa: www.jkt.mil.tz.

Kanali Mlay amesisitiza kuwa nafasi hizo hutolewa bure na ametoa tahadhari kwa jamii kuepuka kudanganywa na matapeli wanaojifanya wasaidizi wa upatikanaji wa nafasi hizo. “Tovuti rasmi ya JKT ndiyo chanzo pekee cha taarifa sahihi. Hakuna ada yoyote inayotozwa,” aliongeza.

Kambi za Kuripoti

Baadhi ya kambi ambazo vijana wanapaswa kuripoti ni:

  • 🪖Kambi za Kanda ya Kati na Kusini: JKT Mpwapwa, JKT Makutupora (Dodoma), JKT Mafinga (Iringa), JKT Mlale (Ruvuma), JKT Nachingwea (Lindi).
  • 🪖Kambi za Kaskazini na Magharibi: JKT Rwamkoma (Mara), JKT Kanembwa, JKT Bulombora, JKT Mtabila (Kigoma), JKT Itaka (Songwe), JKT Milundikwa, JKT Luwa (Rukwa).
  • 🪖Kambi za Pwani na Mashariki: JKT Ruvu, JKT Kibiti (Pwani), JKT Maramba, JKT Mgambo (Tanga).
  • 🪖Kambi za Arusha na Manyara: JKT Makuyuni, JKT Orkolili (Arusha).
  • 🪖Kambi ya Tabora: JKT Mgambo na JKT Msange.

Kwa vijana wenye ulemavu wa kuona, wanapaswa kuripoti katika kambi ya JKT Ruvu, mkoani Pwani, kwa ajili ya mafunzo yao maalum.

Vifaa Muhimu vya Kuripoti

Kanali Mlay ameeleza kuwa vijana wote wanapaswa kuripoti wakiwa na vifaa vifuatavyo:

  • 📌Bukta ya rangi ya dark blue, yenye mpira kiunoni na mfuko mmoja nyuma, isiyo na zipu, yenye urefu unaoishia magotini.
  • 📌Track suit ya rangi ya kijani au blue.
  • 📌Nyaraka zote muhimu za kujiunga na elimu ya juu, ikiwemo cheti cha kuzaliwa.

Kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, Kanali Mlay ametoa wito kwa vijana wote waliomaliza kidato cha sita mwaka huu, kutoka shule za Tanzania Bara, kuhudhuria mafunzo hayo muhimu kwa mujibu wa sheria.