Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imeendelea na msisitizo wake wa kutoitambua Sekretarieti ya uongozi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inayomjumuisha Katibu Mkuu wake John Mnyika.
Sekretarieti hiyo ya CHADEMA iliteuliwa Januari 22 mwaka huu kwenye Baraza Kuu la chama hicho baada ya kupatikana kwa uongozi mpya unaoongozwa na Mwenyekiti wake Taifa, Tundu Lissu.
Hii ni mara ya pili, Ofsisi ya Msajili kutoitambua secretarieti hiyo kwa madai kwamba akidi iliyotumika siku ya uteuzi wake haikutimia, ikikitaka chama hicho kuitishwa mkutano mwingine wa kuidhibitisha secretarieti hiyo kwa kuzingatia matakwa ya katiba na kanuni ya chama hicho.
Malalamiko ya kutokutambua secretarieti hiyo, yaliwasilishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na mmoja wa wanachama wa chama hicho, Lembrus Mchome.
Ofisi hiyo ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika taarifa yake hiyo imeorodhesha majina ya kutowatambua wanachama walio katika secretarieti ya chama hicho kuwa ni John Mnyika, Amani Golugwa, Ali Ibrahimu Juma, Godbless Lema, Dk. Rugemeleza Nshala, Rose Mayemba, Salima Kasanzu na Bwana Hafidhi Ali Saleh
"Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inawasihi wananchi, wadau, mamlaka na taasisi zote za serikali na binafsi, kutowapa ushirikiano na huduma wanachama walioorodheshwa hapo juu, endapo watahitaji kuzipata kama viongozi wa CHADEMA kwa mujibu wa kifungu cha 4(5)(a)(b), 8B, 10(f) vya Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 na Kanuni ya 31 ya Kanuni."
Ofisi hiyo ya Msajili katika taarifa yake kwa umma leo, imeendelea kukisisitiza chama hicho kufanya uamuzi wa busara wa kuitisha kikao halali cha Baraza Kuu la Taifa la chama chao na kujaza nafasi zilizowazi, badala ya kubishana na sheria, kwani sheria ni msumeno.
"Vitendo vya kukaidi maagizo ya Msajili wa Vyama vya Siasa viliendelea kujitokeza ambapo 25 Mei 25, mwaka huu, Makamu Mwenyekiti Bara wa CHADEMA wakati akisoma maazimio ya kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika 23 na 24 Mei, mwaka huu Dar-es salaam alieleza kwamba, kikao hicho kimeazimia kuwa, maamuzi na maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu malalamiko ya Bwana Mchome ni batili na hawatoyafanyia kazi.
"Napenda kuwafahamisha Watanzania kuwa, Msajili wa Vyama vya Siasa amesikitishwa na msimamo huo wa CHADEMA, kwa sababu wanapaswa kufanya uamuzi wa busara wa kuitisha kikao halali cha Baraza Kuu la Taifa la chama chao na kujaza nafasi zilizowazi, badala ya kubishana na sheria, kwani sheria ni msumeno."
Ofisi hiyo imekanusha madai ya CHADEMA kwamba imekuwa ikimsaidia mmoja wa wanachama wa chama hicho, Lembrus Mchome ambaye ndiye alipeleka malalamiko kwenye Ofisi hiyo kwamba secretarieti ya chama hicho iliyochaguliwa kwenye Baraza Kuu Januari 22 mwaka huu, akidi yake haikutimia.
Ofisi hiyo ilisema alichofanya Mchome SI kitu kipya na kwamba vipo vyama vingine viliwahi kuwasilisha malalamiko ya ukiukwajia wa katiba na kanuni ya vyama vyao.
Ofisi hiyo imesema imejitidhisha kuwa alichowasilisha Mchome ni malalamiko na siyo rufani kama inavyodaiwa na chama hicho.
Kuhusu kauli iliyotolewa na CHADEMA kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama va Siasa hana mamlaka ya kufanyia kazi malalamiko ya mwanachana wa chama Cha siasa yanayohusu ukiukwaji wa katiba na kanuni za chama na kutoa maelekezo, Ofisi hiyo imesema ilitia ufafanuzi wa kina kuhusu suala hilo katika barua iliyokiandikia chama hicho.
Kadhalika, Msajili wa Vyama vya Siasa amesitisha ruruku kwa chama hicho mpaka pale watakapotekeleza maelekezo yake.
"Kutokana na ombwe la uongozi wa chama hicho,Msajili wa Vyama vya Siasa ameamua kusitisha kuwapa ruzuku chama hicho hadi kitakapotekeleza maelekezo kwa sababu chama hicho hakina viongozi wanaoweza kusimamia mapato na matumizi na marejesho ya fedha hizo za umma."
Kwa mujibu wa Msajili wa Vyama vya Siasa, kama wataendelea kukaidi, atazitaka mamlaka husika kuchukua hatua za kijinai dhidi ya wanachama hao ambao anadai wanaojifanya viongozi, kutokufanya shughuli za kisiasa.
Pia, anasema anayo mamlaka ya kusimamisha usajili wa chama hicho endapo kitaendelea kuwatambua wanachama hao ambao Ofisi yake haiwatambui kama viongozi chama hicho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED