TAKUKURU yabaini viongozi AMCOS kupiga milioni 151 za wakulima wa tumbaku

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:43 PM May 27 2025
Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy akitoa taarifa ya Taasisi hiyo kwa vyombo vya habari.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy akitoa taarifa ya Taasisi hiyo kwa vyombo vya habari.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Shinyanga, imebaini unadhilifu wa fedha sh.milioni 151, fedha za Wakulima wa zao la Tumbaku halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, kutoka kwa viongozi wa AMCOS.

Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy,wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Amesema kwa kipindi cha robo ya tatu kuanzia Januari hadi March 2024/2025, Taasisi hiyo ilibaini ubadhilifu wa fedha sh.milioni 151, fedha za malipo ya wakulima wa zao la Tumbaku katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama.

Amefafanua kuwa fedha hizo zimefujwa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Msingi cha Ushirika AMCOS ya Ibambala Halmashauri ya Ushetu, ambazo zilikuwa ni kwa ajili ya malipo ya fidia kwa Wakulima ambao walipata hasara kutokana na mafuriko yaliyoharibu uzalishaji Tambaku katika msimu wa kilimo 2023/2024.

Amesema katika ufuatiliaji wao, walibaini kwamba fedha hizo hazikugawanywa kwa wakulima,na badala yake viongozi wa chama hicho walizitafuna fedha hizo.

Amewataja viongozi hao kuwa ni Mwenyekiti wa AMCOS hiyo Faida Paulo aliyejilipa sh.milioni 53, Katibu wa Chama hicho Charles Shiyego aliyechukua milioni 58,Mke wa Katibu huyo Lucy Gidabita aliyelipwa milioni 34,na Mtoto wa Katibu Charles Charles aliyelipwa milioni 5.5 kinyume na taratibu.

"Baada ya Takukuru kulifuatilia suala hili la ubadhilifu wa fedha tumefanikiwa kurejesha kiasi cha sh.milioni 92.2 fedha ambazo zilikuwa zimefujwa kati ya milioni 151.5 na viongozi hawa wa AMCOS,"amesema Kessy.

Ameongeza kuwa bado wanaendelea na uchunguzi ili kuzirudisha fedha zote zitimie sh. milioni 151, kwamba  baada ya kukamilika viongozi hao pia watafikishwa Mahakama.

Katika hatua nyingine, amesema walifanya ufuatiliaji wa miradi 9 ya maendeleo yenye thamani ya sh.bilioni 2, ili kuzuia mianya ya Rushwa na kujengwa chini ya kiwango, na kwamba kwa dosari walizozikuta walitoa maelekezo mapungufu hayo yafanyiwe kazi.

Ametoa wito kwa wananchi wa Shinyanga, kwamba wanapoona mianya ya Rushwa au kuombwa Rushwa watoe taarifa ili hatua za haraka zipate kuchukuliwa.