MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Daraja la Kigogo-Busisi maarufu kama Daraja la JPM lipo tayari kwaajili ya matumizi na kuwa muda wowote kuanzia sasa watu wataruhusiwa kupita wakati likisubiri kuzinduliwa.
Msigwa amebainisha jana katikati ya daraja hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari alioambatana nao kwaajili ya ukaguzi wa miradi mbari mbali ya maendeleo inayotekelezwa katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga.
Alisema daraja hilo linalounganisha Wilaya mbili za Sengerema na Misungwi linaunganisha pia mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Alisema kuanza kutumika kwa daraja hilo kutafungua fursa za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni katika mataifa pamoja na mikoa yote inayounganishwa na daraja hilo.
“Kwa sasa wananchi wanalazimika kutumia hadi saa nne kusubiri na kusafiri kwa vivuko vyetu tulivyo navyo katika eneo hili ambavyo wakati mwingine vinazuiliwa na ongezeko la gugumaji na kusabaisha usumbufu mkubwa,”alisema.
Aidha, alisema mpaka sasa Mradi huo umefikia asilimia 99 ukibakiwa na shughuli chache ambazo haziathiri usafiri na usafirishaji katika daraja hilo.
Alisema shughuli hizi zinahusisha uchorwaji wa maeneo ya wavukao kwa miguu pamoja na kuweka kingo katika barabara za kuunganisha daraja hilo.
“Kimsingi ujenzi umekamilika hapa wakati wowote Waziri wa Ujenzi atapeperusha kibendera katikati ya mwezi huu watu waanze kupita wakati tunasubiri Rais Samia Suluhu Hassani kufanya uzinduzi,” alisema Msigwa.
Alisema wakati Rais Samia anapokea madaraka mradi huo ukiwa asilimia 25 lakini ndani ya miaka mine ameendelea kutoa fedha hadi unakamilika.
Alisema daraja hilo ambalo kwa shughuli zote limegharimu zaidi ya Sh.bilioni 700 litakuwa na uhai wa miaka 100 na kuwa likiendelea kuboreshwa litaishi miaka mingi zaidi.
Msimamizi wa daraja hilo kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADs), Mhandisi Willium Sanga alisema hadi sasa mkandarasi tayari amelipwa fedha zaidi ya Sh.bilioni 530 na kuwa hakuna fedha anayodai.
“Mradi huu una urefu wa kilomita tatu na upana wa mita 28.45, barabara unganishi kilometa 1.66 chini ya ufadhili wa serikali kwa asilimia 100,”alisema Mhandisi Sanga.
Aidha alisema gharama za mkandarasi wa daraja hilo ni Sh.bilioni 592.6 na Mhandisi Mshauri Sh.bilioni 12.16 na kuwa fedha nyingi zililipwa kama fidia kwa wananchi waliokuwa katika eneo hilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED