Jeshi la Polisi Mbeya lakanusha kumkamata Mdude

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 04:12 PM May 02 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP, Benjamani Kuzaga.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP, Benjamani Kuzaga.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, limekanusha madai ya kuhusu kumkamata Mpaluka Nyagali maarufu Mdude ambaye taarifa zimesambaa kwamba usiku wa kuamkia Mei 2, 2025 amekatwa na watu wasiojulikana waliojitambulisha ni maofisa wa polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP, Benjamani Kuzaga, amesema Mei 02, 2025 majira ya asubuhi lilipokea taarifa kutoka kwa Sije Mbugi (31) mkazi wa Iwambi ambaye ni mke wa Mpaluka  Nyagali  maarufu Mdude kuwa majira  usiku wa Mei Mosi, 202 wakiwa wamelala huko Mtaa wa Ivanga, Kata ya Iwambi Jijini Mbeya kuwa watu wasiofahamika waliwavamia baada ya kuvunja mlango na kuingia ndani na kisha kumjeruhi Mdude sehemu mbalimbali za mwili wake.

Ameeleza  kuwa watu hao baada ya tukio hilo walifanikiwa kutoweka na mhanga na kwenda naye kusikojulikana.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linakanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikidai Askari Polisi kuhusika na tukio hili, tunaendelea na ufuatiliaji ili kumpata mhanga na kuwabaini waliohusika katika tukio hili kwa hatua zaidi za kisheria.


Amesema Polisi  wanatoa  wito  kwa mwananchi mwenye taarifa za mahali alipo Mdude azitoe ili kufanikisha kumpata pamoja na taarifa za watu waliohusika katika tukio hili ili waweze kukamatwa.