Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile akizungumza na waandishi wa habari.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amewaasa waandishi wa habari kuwa makini wanaporipoti kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini na uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kuzingatia utaratibu rasmi wa kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 2, 2025 jijini Dar es Salaam, Balile amesema kuwa miongoni mwa masharti ya kufuata ni kuwa na kitambulisho halali cha kazi pamoja na kuvaa jaketi maalum linaloonesha kuwa mhusika ni mwandishi wa habari.
“Mwandishi hapaswi kuzuiwa kufanya kazi yake ya kuujulisha umma, hasa katika kesi nyeti kama ya Tundu Lissu, kwani jamii nayo ina haki ya kujua kinachoendelea,” amesema Balile. 1
Ameongeza kuwa tayari TEF imekutana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro , ambapo walikubaliana kuwa waandishi waruhusiwe kuingia kusikiliza kesi hiyo, lakini kwa masharti ya kuzingatia taratibu zinazojulikana.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam, Bakari Kimwanga, amewakumbusha waandishi kuzingatia usalama wao binafsi wanapotekeleza majukumu yao katika maeneo ya mahakama na kwenye matukio yenye hisia kali.
“Swala la usalama linaanza na wewe kabla ya mtu yeyote. Unapoanza kutekeleza majukumu yako, unapaswa kufuata taratibu zote ili kupunguza changamoto zinazoweza kukukuta ukiwa kazini,” amesema Bakari.