Chalamila: Shambulio la Padri Kitima lisihusishwe na serikali, mamlaka zake

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:10 PM May 02 2025
news
Mtandao
Mta

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema shambulio la Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), lisihusishwe na yeyote kwa kuwa hata yeye akiwa anafanya mazoezi aliwahi kuvamiwa na vibaka wakitaka kumpora simu.

Aidha, amesema tukio la kushambuliwa Dk. Kitima lisiangaliwe kwa upande bali watu wasimame katikati kwa kuwa linaweza kumkuta mtu yeyote, hata Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya,  mwandishi wa habari au kiongozi yoyote.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 2,2025, Chalamila amesema:“Sioni maana ya hata kidogo ya ama serikali, au jambo lolote la kisiasa kufurahia shambulio hili ambalo limetokea kwa kiongozi wetu wa dini, mwalimu wetu, mwanaphilosofia na mwanathelojia na mragibishi wetu mkubwa.”

Amesema siku tatu zilizopita akiwa anafanya mazoezi walitokea vijana wakidhani yuko peke yake wakitaka kumpora simu.

“Naamini wangefanikiwa kunipora na kufanikiwa kunijeruhi, lazima baadhi ya watu wangetamka maneno ambayo si ya kweli, wangeweza kusema wabaya wa Chalamila wamemdhuru Chalamila, watu wa vyama vya upinzani. 

Lakini kiukweli ingelikuwa ni kibaka kama kibaka mwingine ambaye alidhani anamuibia mtu mwingine na hakujua nina walinzi, kibaka yule alipelekwe kituo cha polisi na kuchukuliwa hatua.”

Kwa mujibu wa Chalamila, amelielekeza Jeshi la Polisi kuongeza wigo wa ulinzi wa watu na mali zao pamoja na umakini kwamba kwa nyakati kama hizi watu wanafanya jambon a kuhamisha kwamba limefanyika kwasababu ya jambo fulani.