Mkazi wa Kijiji cha Mbati, Kata ya Mbati, Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Marimu Simba, amelazwa katika Hospitali ya Missioni ya Mbesa kwa ajili ya matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya na tembo.
Tukio hilo limethibitishwa na kaka wa majeruhi huyo, Issa Mtila, ambaye alisema kuwa lilitokea Aprili 29, 2025, majira ya saa 5 asubuhi katika maeneo ya Kitongoji cha Jembe wakati walipokuwa wakielekea Dhamani.
Kwa mujibu wa Mtila, baada ya tukio hilo, walifanikiwa kumpata ndugu yao akiwa hai lakini amejeruhiwa vibaya na alikuwa amejificha ndani ya mafukutu ya miti. Walimbeba na kumpeleka hadi mashamba ya karibu kisha wakawasiliana na kijiji kuomba msaada wa usafiri wa pikipiki ili kumpeleka hospitalini.
Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa Kata ya Mtina, Rashid Swalehe maarufu kwa jina la Tayson, alithibitisha kulifahamu tukio hilo na kueleza kuwa mara baada ya kupata taarifa alituma pikipiki mbili kumfuata majeruhi katika eneo la tukio na kumpeleka katika Zahanati ya Kijiji cha Mbati.
Diwani Swalehe alisema kuwa baada ya uchunguzi wa awali uliofanywa na maafisa tabibu wa zahanati hiyo, walishauriwa kumpeleka manusura huyo katika hospitali kubwa kwa ajili ya matibabu zaidi, ndipo walikubaliana kumkimbiza Hospitali ya Missioni ya Mbesa.
Aliendelea kueleza kuwa katika hatua za awali za ufuatiliaji wa tukio hilo, alitoa taarifa kwa Mkuu wa Kituo cha Makiasiri kilichopo Tarafa ya Nalasi, Kijiji cha Mbesa, pamoja na kumjulisha Afisa Wanyamapori wa wilaya kwa ajili ya hatua za kisheria na ufuatiliaji wa mnyama huyo hatari.
Swalehe alibainisha kuwa walipewa ushirikiano mkubwa kutoka kwa mamlaka husika, ikiwa ni pamoja na kupokea manusura huyo hospitalini na kugharamia huduma zote za matibabu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED