Msukuma atishia kushika shilingi Bajeti ya Madini

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 04:49 PM May 02 2025
Msukuma atishia kushika  shilingi Bajeti ya Madini
Picha: Nipashe
Msukuma atishia kushika shilingi Bajeti ya Madini

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku Msukuma, ametishia kushikilia bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2025/2026 endapo Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, hatatoa majibu kuhusu utaratibu wa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zinazotakiwa kurejeshwa na kampuni za uchimbaji wa madini.

Ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, akieleza kuwa halmashauri yake inadai kiasi cha Shilingi bilioni 23 kutoka kwa kampuni hizo, fedha ambazo zilitakiwa kutumika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.

“Fedha hizi ni nyingi sana, nataka nipate majibu, kwa nini hadi leo hatujapatiwa? Kampuni hizi za uchimbaji hawataki kuzitoa kwa halmashauri ili zitekeleze miradi ya maendeleo. Wanataka wao ndiyo wasimamie utekelezaji na kufanya manunuzi yote,” amesema Msukuma kwa ukali.

Alisisitiza kuwa fedha hizo ni haki ya wananchi na kwamba ni lazima wizara ieleze utaratibu wa utekelezaji wa miradi hiyo kupitia fedha za CSR ili kuondoa mkanganyiko wa kisheria na kiutendaji kati ya kampuni na halmashauri husika.