BoT yaonya matumizi ya fedha za kigeni kwa huduma ndani ya nchi

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 10:57 AM May 03 2025
news
BoT
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imewaonya wananchi wanaotumia fedha za kigeni ndani ya nchi kwa ajili ya huduma mbalimbali, kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika.

Taarifa kwa umma iliyotolewa Mei 2, 2025 na BoT, inaeleza kuwa kanuni za matumizi ya fedha za kigeni za mwaka 2025 zinaeleza kuwa bei na malipo ya bidhaa na huduma zote ndani ya nchi zinapaswa kufanyika kwa Shilingi ya Tanzania. 

“Hivyo, ni kosa kunukuu, kutangaza au kubainisha bei kwa kutumia fedha za kigeni; kulazimisha, kuwezesha au kupokea malipo kwa fedha za kigeni; au kukataa malipo kwa Shilingi ya Tanzania,”imefafanua taarifa hiyo iliyosainiwa na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.

Aidha, Kanuni hizo zilizochapishwa katika Gazeti la Serikali namba 198 la Tarehe 28 Machi 2025, zimeanisha miamala ambayo imeruhusiwa kufanyika kwa fedha za kigeni. 

Aidha, Kanuni zimeweka ukomo wa muda kwa mikataba inayotekelezwa kwa fedha za kigeni na kuweka katazo la kutokuingia au kuhuisha mikataba inayotaka malipo yafanyike kwa fedha za kigeni kuanzia tarehe 28 Machi 2025.

“Wageni kutoka nje ikiwemo watalii watabadili fedha za kigeni kupitia benki za biashara na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini au kuendelea kufanya malipo kwa kutumia kadi za kielektroniki au utaratibu wa kawaida wa kidigitali,”imefafanua.

Pia, imewataka wananchi kutoa taarifa za ukiukwaji wa Kanuni hizi kupitia barua pepe: fx.regulations@bot.go.tz, Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU). Jeshi la Polisi, au mamlaka nyingine yoyote ya utekelezaji wa sheria kwa hatua stahiki.