MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa(UVCCM) wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Rehema Sombi amesema ameridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa Chuo cha ufundi stadi halmshauri ya Msalala Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, kinachogharimu zaidi ya Sh.bilioni 3.5 fedha kutoka serikali kuu na wadau.
Sombi ameyabainisha haya leo baada ya kupokea taarifa fupi ya ujenzi wa chuo hicho kutoka kwa Mkuu wa chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mwanva(Mwanva FDC) Gastoni Chiwalanga, unaotekelezwa katika kijiji cha Bunango kata ya Bugarama halmashauri ya Msalala kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari 16 zilizotolewa na serikali ya kijiji.
Chiwalanga akitoa taarifa ya ujenzi amesema, ujenzi wake ulianza Mei 30 mwaka 2022 na unatarajia kukamilika mwakani 2026 kwa gharama ya Sh.bilioni 3.5 kati yake Sh.milioni 368.272 ni fedha zilizotengwa kwenye mfuko wa CSR na halmashauri ya Msalala.Amesema,awamu ya kwanza mradi unakadiriwa kutumia kiasi cha Sh.bilioni 1.686 na mpaka sasa umetengewa Sh.bilioni 1.481 ambapo utajumuisha ujenzi wa majengo tisa, ambayo ni Karakana tatu, jengo la utawala, Madarasa na Tehama, nyumba ya mkuu wa chuo, kibanda cha mlinzi na jengo la kupokelea umeme na choo cha nje.
Aidha amesema, wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa umeme na maji hivyo kupelekea gharama za matunizi ya maji kuwa kubwa, na kuiomba serikali kuangalia namna ya kufikisha huduma ya maji kutoka Ziwa Victoria ili mradi utakapokamilika na kuanza kazi wanachuo wasipate shida.
Awali Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Rehema Sombi amesema, ameridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa chuo hicho na kuwataka wasimamizi wake kuhakikisha thamani za majengo ziendane na fedha zilizotolewa na setikali pamoja na wadau.
Amesema, Serikali ya Dk.Samia Suluhu Hassani imeweka kipaumbe sana katika sekta ya elimu na sasa inajenga chuo hicho ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na kujiajiri na kuondokana na dhana ya kutegemea ajira kutoka serikali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED