Wenyeviti wa vijiji 92 wapewa baiskeli za ufuatiliaji miradi

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 10:35 AM May 04 2025
Mbunge wa Msalala, Iddi Kasim akizungumza wakati wa kukabidhi baiskeli kwa wenyeviti wa serikali za vijijini jimboni kwake leo.
PICHA: SHABAN NJIA.
Mbunge wa Msalala, Iddi Kasim akizungumza wakati wa kukabidhi baiskeli kwa wenyeviti wa serikali za vijijini jimboni kwake leo.

MBUNGE wa Jimbo la Msalala mkoani Shinyanga, Iddi Kasimu amewapatia usafiri wa baiskeli bure wenyeviti wa serikali ya vijiji 92 vya halmashauri ya Msalala, utakaowasaidia kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao zenye thamani ya Sh.milioni 23.

Baiskeli hizo zimekabidhiwa leo na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Kawaida, baada ya kuwahutubia wananchi wa kata ya Bugarama halmashauri ya Msalala na kuwaeleza namna serikali inavyotekeleza miradi inayogusa maisha ya wananchi huku akiwasisitiza kuilinda na kuitunza ili iwanufaishe.

 Amempongeza mbunge kwa kuona umuhimu wa kuwapatia usafiri wenyeviti wote wa serikali za mitaa kwa lengo moja la kufautilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwataka wengine kuiga mfano huo ili kuwa pamoja na viongozi wao ambao kwa asilimia kubwa wako karibu na wananchi.

 “Ninakupongeza sana kwa hatua hii ya kuwafikia wenyeviti wa serikali za mitaa na kuwapatia usafiri, tangu nimeanza ziara yangu ya siku 10 sijakutana na tukio la namna hii; Wenyeviti tumieni baiskeli hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ”ameongeza Ali.

Baadhi ya Baiskeli zilizotolewa na Mbunge wa Msalala, Iddi Kasimu.

 Awali Mbunge  Iddi Kasimu amesema, ametoa usafiri huo ili kuwawezesha wenyeviti wa serikali za vijiji kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea na pale watakapoona kuna shida basi watoe taarifa mapema ili hatua zichukuliwe.

 Amesema, kila baiskeli moja imegharimu Sh.250,000 sawa na jumla ya Sh.milioni 23 na kuwataka zitumike katika matumizi sahihi, kwani kwenye maeneo yao kuna miradi inatekelezwa na inahitaji ufuatiliaji wa hali ya juu na kuahidi kushirikiana nao katika kuwafikishia maendeleo wananchi.

wanachama.JPG 136.24 KB

 Wakati huo huo; Wanachama tisa (9) wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Kahama wametimkia CCM na kupokelewa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Ali Kawaida katika Mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Bugarama-Msalala.

 Wanachama hao waliongozana na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati tendaji ya wilaya ya Kahama wa Chadema, Samson Thomas, amesema, wameondoka kwenye chama chao na kujiunga na CCM kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kuwafikishia maendeleo wananchi.

Hata hivyo ameahidi kuwa mtii na msikivu wakati wote akiwa CCM na kuahidi kushiriki kikamilifu katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na atakapokosa nafasi atashirikiana na atayechaguliwa katika kuwafikia wananchi na kuwahudumia.