VIONGOZI wa dini wa madhebu mbalimbali nchini wameshauriwa kutojihusisha na siasa na wala kuwa sehemu ya wachochezi kwakuwa wadhifa wao unawafanya kuwa kimbilio la wengine pale nchi inapokumbwa na changamoto, huku wakikumbushwa wajibu wa kuliombea taifa hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Hayo yalielezwa jana na Wachungaji kutoka Tanzania na Kenya wa Kanisa la Wadventista Wasabato walipokuwa wakihitimisha Wiki ya Uamsho iliyoandaliwa na Kwaya ya Gethsemane Group Kinondoni (GGK) ikikusudia kuliombea Taifa amani umoja na mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumza baada ya kuhitimisha maombi hayo Katibu wa Jimbo la Mashariki Kanisa la Waadvestita Wasabato Tanzania Mchungaji Shashi Wanna, alitoa wito pia kwa waumini wa dini mbalimbali ambao ni wanasiasa kufanya kampeni za kistaarabu, akisisitiza kuwa kila mmoja anajukumu la kuhakikisha amani, umoja na mshikamano unadumishwa.
“Tulikuwa na wiki ya uamsho wa kiroho katika kanisa letu lakini pia kuliombea Taifa letu na Wachungaji wenzetu kutoka Kenya ambao tulikuwa nao wenzetu wanauzoefu mkubwa wa mambo ya siasa yanayoendelea Kenya. Tumehimiza maombi na umuhimu wa amani katika nchi yetu.
“Bila amani nchi haiwezi kutawalika lakini sisi kama Wakristo bila amani hatuwezi kufanya kazi ya Injili, hatuwezi kupata uhuru wa kuabudu, tumeshirikiana kuliombea Taifa letu nasi kama Watanzania tunawashukuru wachungaji wenzetu maana wamekuja kutuamsha kutuonyesha umuhimu wa maombi na kumtegemea Mungu,” alisema Mchungaji Wanna.
Aliongeza kuwa kanisa hilo linatoa rai kwa waumini wao kuendelea kuliombea Taifa hasa mwaka huu wa uchaguzi na kama kanisa hawataingia kwenye siasa, huku akihadharisha waumini wao wanaojihusisha na suala hilo kufanya siasa za kistaarabu.
Aidha, Mchungaji Wanna alishauri waumini wao wawe ni wenye kusamehe na kujishusha, huku akisisitiza viongozi wengine wa dini nchini kutokuwa sehemu ya uchochezi badala yake wawe sehemu ya kuleta amani kwa maombi na ushauri.
Mchungaji Patrick Muthee kutoka Kenya alieleza kuwa katika zama hizi ambazo Dunia imeharibika wakati mwingine makanisa na waumini wake wanajaribiwa, na kwamba kanisa linapoingia kwenye siasa kunakuwa na changamoto kwasababu imani ya kiroho inaondoka.
“Kazi ya kanisa ni kuleta watu pamoja na tunatambua viongozi Mungu ndio huchagua sisi kama waumini anatutumia katika hali ya kupiga kura lakini Mungu anajua njia iliyobora. Hivyo kama kanisa viongozi, wachungaji, na masheikhe tuzungumze na waumini wetu.
“Tuwaambie jukumu kubwa la kuchagua viongozi ni la Mungu hivyo tumtangulize Mungu, wawe na imani Mungu ndiye anatuchagulia viongozi hatutakuwa na mashindano, hatutakuwa na vurugu,” alisisitiza Mchungaji Muthee.
Pia alionyesha msisitizo akisema: “Tunawaomba watulie na siku ya kupiga kura wajue kila mmoja ni ndugu wa mwenzie wale waliko upinzani, na waliko serikalini wote ni wamoja, na atakayechaguliwa awe wa upinzani au chama tawala yeye ni mmoja wa wale waumini na raia wa nchi moja.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED