Hapi: Vijana zungumzeni mazuri yaliyofanywa na Serikali

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 08:20 AM May 04 2025
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi, Ally Hapi.
PICHA: RENATHA MSUNGU
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi, Ally Hapi.

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi, Ally Hapi,ameutaka Mtandao wa vijana wa Kesho Yetu,Uzalendo Wetu na Utaifa (TK Movement),kutokatishwa tamaa na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya serikali,badala yake wasonge mbele kulisemea taifa kwenye mambo mazuri linayofanya.

Hapi amesema hayo  jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya vijana zaidi ya 600 wa  mtandao wa TK Movement kutoka mikoa yote hapa nchini kujifunza kuhusu masuala ya ushiriki wa uchaguzi Mkuu.

Amesema,vijana hao wasikubali kurudishwa nyuma katika kile ambacho wanakifanya ili kuhakikisha serikali inasikika kwa wananchi,kwa sababu hakuna jambo zuri linalofanywa bila ya kupata kikwazo kutoka kwa wengine.

"Msikubali kukata tamaa kutokana na vikwazo mnavyokutana navyo kwenye utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku,fanyeni kazi kwa weledi ili kuisemea serikali kutokana na miradi ya maendeleo inayofanya,"amesema Hapi.

Hata hivyo aliuhakikishia Mtandao wa TK Movement ya kuwa atayafanyia kazi malalamiko yao yote,yakiwemo maombi ya kupata ushirikiano wa utendaji kazi wao katika mikoa mbalimbali ambayo wanakwenda kuwajibika kwa ajili ya serikali.

"Nimeyasikia malalamiko yenu nimeyachukua na nitayafanyia kazi,kikubwa nanyie fanyeni kazi mliyopanga kuifanya kwa ajili kulitangaza taifa,"alisema Hapi.

Mbali na hayo aliutaka mtandao huo kujikita pia katika masuala ya kiuchumi huku akiwasisitiza kuanzisha Benki ambayo itatumika kukopesha vijana na jamii kwa ujumla ili kujiinua kiuchumi wao na familia zao.