Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mbeya kimeendelea kumtafuta kada wake Mpaluka Said maarufu Mdude aliyepotea tangu usiku wa kuamkia Mei 2 mwaka huu.
Katibu wa chama hicho kanda ya Nyasa, Grace Shio akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo jana, amesema licha ya viongozi wa chama hicho kwenda na picha ya mtu wallyedai ni askari wanayemtuhumu kuhusika na uvamizi wa Mdude polisi wamekana kumtambua mtu huyo kama mtumishi wao.
Katibu huyo ameeleza hayo wakati akizungumza nje ya ofisi ya makao makuu ya polisi mkoa wa Mbeya baada ya kuandamana kutoka ofisi za chama hicho kanda ya Nyasa hadi katika ofisi hiyo kwa lengo la kutaka kujua alipo Mdude.
Juzi Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya SACP, Benjamini Kuzaga alikanusha taarifa zilizosambaa mapema katika mitandao ya kijamii zikidai Mdude alikamatwa na makachero wa Jeshi la Polisi. Alisema hakukuwa na tukio lolote ambalo linalilazimisha Jeshi la Polisi kumkamata mtu huyo.
Kamanda Kuzaga alisema taarifa za tukio hilo zililifikia Jeshi la Polisi asubuhi kupitia mke wa Mdude aitwaye Sije Mbugi (31), ambaye ametaarifu kuwa wahalifu hao waliwavamia wakati wamelala.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED