TANZANIA huzalisha kati ya tani milioni 14.4 hadi 20.7 za taka kila mwaka, hali inayosababisha changamoto ya usimamizi wa taka.
Miji mikubwa kama Dar es Salaam inaongoza kwa uzalishaji wa taka, ikichangia asilimia 15.3 ya taka zote nchini, nyingi huishia baharini, kuharibu ikolojia ya majini na kuhatarisha afya za binadamu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Mei 3, 2025, wakati wa zoezi la usafi wa fukwe ya Mbezi B, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, amesema licha ya changamoto hizo, bado kuna fursa nyingi za kuibadili sekta hiyo kuwa chanzo cha ajira, uchumi na uhifadhi wa mazingira.
Katika kukabiliana na tatizo la uchafuzi wa fukwe, amesema Serikali imechukua hatua madhubuti kwa kutunga Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 inayolenga kukabiliana na changamoto hizo.
Imeandaliwa mikakati ya kimazingira ya muda mrefu wa mwaka 2022-2032 inayojumuisha mfumo wa uchumi wa mzunguko (circular economy) ili kushughulikia taka kwa njia endelevu.
Ameongeza kuwa wanaendelea kuandaa mwongozo wa uwekezaji katika usimamizi wa taka, ambao umehamasisha zaidi ya kampuni 257 na watu 99 nchini kuingia katika sekta ya ukusanyaji, usafirishaji na uchakataji wa taka ngumu, ikiwemo taka za plastiki, chupa, metali chakavu na vifaa vya kielektroniki.
“Kampuni hizi zimeanza kuchakata taka kuwa bidhaa zenye thamani kama mbolea, mkaa mbadala, na bidhaa nyingine rafiki kwa mazingira. Hii ni fursa ya biashara, ajira, na suluhisho la muda mrefu,” ameongeza Waziri Masauni.
Katika kuimarisha usafi wa fukwe, Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Patrick Nyamvumba, ameeleza dhamira ya kuendelea kushirikiana na wadau katika kuhakikisha fukwe za Dar es Salaam zinatunzwa.
Naye Mkurugenzi wa Watetezi wa Haki za Binadamu Afrika (AHRN), Olivier Muhizi, amesema wamedhamiria kujenga kituo kikubwa cha urejelezaji wa taka eneo la Mbezi Beach.
Amesema kituo hicho kinatarajiwa kukamilika na kuanza kufanya kazi ndani ya miezi miwili kwa ufadhili wa Balozi wa Saudi Arabia ambao wametoa kiasi cha sh. milioni 200 huku serikali ikitoa eneo kwa ajili ya ujenzi.
“Tumejipanga kuanzisha kituo cha urejelezaji wa taka ambacho kitachambua taka, kuziongezea thamani na kuzalisha bidhaa kama mbolea na mkaa mbadala. Lengo ni kuwa na mzunguko wa taka wenye tija kwa jamii na mazingira,” amesema Muhizi.
Amezungumzia changamoto ya uchafuzi wa fukwe kuwa ni ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu utunzaji wa fukwe, uharibifu wa mazingira ya bahari kutokana na plastiki zinazomezwa na samaki, na kutokuwepo kwa miundombinu ya kisasa ya uchakataji wa taka.
Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Yahya Okeich, amesema ushiriki wa kila mwananchi katika Usafi wa fukwe itasaidia kuimarisha sekta ya utalii wa baharini, kuvutia wawekezaji na utunzaji wa mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule , amesema wilaya hiyo ina fukwe zenye urefu wa kilomita 42 zinazotumika kwa biashara, utalii wa bluu, uvuvi na burudani.
Amesema vijana wanaotumia teknolojia kuchakata taka kuwa bidhaa kama kalamu na mifuko rafiki wa mazingira wanapaswa kuungwa mkono zaidi, kwani wanachangia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kukuza afya ya jamii na kuongeza ajira.
Tani 700 za taka zikiongoza za plastiki zimekusanywa katika fukwe ya Mbeya Beach B wakati wa zoezi la usafi lililofanyika Mei 3, 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED