Barabara ya Mlandizi kwenda SGR kujengwa kwa Sh. bilioni 60.25

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:32 PM May 02 2025
Barabara ya Mlandizi kwenda SGR kujengwa kwa Sh. bilioni 60.25
Picha: Mpigapicha Wetu
Barabara ya Mlandizi kwenda SGR kujengwa kwa Sh. bilioni 60.25

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani umesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Mlandizi hadi kituo cha reli ya kisasa (SGR) kilichopo Ruvu Station yenye urefu wa kilomita 23, kwa gharama ya Shilingi bilioni 60.25.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Kibaha, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani, Baraka Mwambage, amesema kuwa mkataba huo umesainiwa kati ya TANROADS na mkandarasi Dott Services Limited na kazi hiyo inatarajiwa kutekelezwa ndani ya kipindi cha siku 900.

Mwambage amesema kuwa ujenzi huo utahusisha vipande viwili vya barabara ambapo kipande cha kwanza ni cha kilomita 15 ndani ya barabara ya mkoa ya Mlandizi – Manerumango, na kipande cha pili chenye urefu wa kilomita 8 kitaanzia makutano ya barabara hiyo hadi kituo cha reli ya SGR.

“Mradi huu pia utahusisha ujenzi wa madaraja manne pamoja na uwekaji wa taa za barabarani kuanzia Mlandizi Mjini hadi kituo cha SGR, jambo litakaloboreshwa usalama na urahisi wa usafiri kwa wananchi,” amesema Mwambage.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Dott Services Limited, Golamudivet PrudhuitRaj, alisema wako tayari kuanza kazi mara moja na watahakikisha wanatekeleza mradi huo kwa mujibu wa mkataba na ndani ya muda uliopangwa.

Ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuondoa changamoto kubwa ya usafiri kwa wananchi wa Mlandizi na maeneo ya jirani wanaotumia treni ya SGR, ambao kwa sasa hulazimika kutumia usafiri wa pikipiki (bodaboda) kwa gharama ya kati ya Sh 4,000 hadi 5,000 kufika kituoni.

Wananchi wameeleza matumaini yao kuwa barabara hiyo itarahisisha safari na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo, huku ikiimarisha miundombinu ya usafiri kati ya miji na vituo vikuu vya reli.