Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk. Tulia Ackson, ametangaza rasmi nia ya kugombea ubunge katika jimbo jipya la Uyole, mkoani Mbeya, katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza leo Mei 23, 2025, wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Wilaya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Tulia amesema amefikia uamuzi huo baada ya kuona kasi ndogo ya maendeleo katika eneo hilo, hali inayowalazimu wananchi kusubiri kwa muda mrefu kupata huduma stahiki.
“Maendeleo ya Uyole yanasonga kwa taratibu sana. Nimeamua kujitoa kwa moyo wote ili kuhakikisha wananchi wa Uyole wanapata huduma wanazostahili na maendeleo ya haraka,” amesema Dk. Tulia.
Akitumia nafasi hiyo kuomba ridhaa ya wanachama wa CCM, Dk. Tulia amewahimiza viongozi na wanachama kuchagua kiongozi atakayekuwa mtumishi wa kweli wa wananchi na si mtu wa kutafuta maslahi binafsi.
“Nitoe wito kwenu, watu wengi watakuja kwenu, lakini chagueni kiongozi. Chagueni mtumishi. Hilo litasaidia sana kuyakimbiza maendeleo ya jamii,” ameongeza.
Jimbo la Uyole ni miongoni mwa majimbo mapya yaliyoundwa katika marekebisho ya mipaka ya kisiasa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, na linatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na idadi ya wakazi na umuhimu wake kiuchumi ndani ya Mkoa wa Mbeya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED