Serikali kujenga Kituo kikubwa cha Kibingwa cha moyo MUHAS

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 08:21 PM May 23 2025
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Jumuiya ya Afrika Mashariki, itajenga kituo cha kibingwa cha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu katika Kampasi ya Mloganzila ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya Mradi wa Kituo cha Umahiri cha Afrika Mashariki, Prof. Mkenda alisema mradi huo utagharimu Shilingi bilioni 224, na utaifanya Tanzania kuwa kinara wa huduma za kibingwa kwa moyo katika kanda ya Afrika Mashariki.

“Kupitia mradi huu, Tanzania itaongeza wataalamu wa afya, kuboresha huduma na kuimarisha tafiti za magonjwa ya moyo na mishipa ya damu,” amesema Prof. Mkenda.

Kaimu Mkurugenzi wa Mradi huo, Dk. Rodrick Kisenge, amesema awamu ya kwanza ya mradi ilihusisha mafunzo kwa wataalamu na tafiti, huku awamu ijayo ikilenga kujenga miundombinu ya kisasa ya matibabu na utafiti.

Amesema Afrika ina uhaba mkubwa wa wataalamu wa moyo, ambapo kuna daktari mmoja tu wa upasuaji kwa kila watu milioni 25 katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, hali inayosababisha watoto wengi kushindwa kupata matibabu kwa wakati.

Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Apolinary Kamuhabwa, amesema kituo hicho kitapunguza mzigo wa magonjwa ya moyo nchini, wakati Mkuu wa MUHAS, Prof. David Mwakyusa, alisisitiza kuwa tafiti zitakazofanyika zitalenga kutatua changamoto za kiafya za wananchi.