Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, CPA Amos Makalla, amekiombea kura za kishindo Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu ujao, akiwaeleza Watanzania kuwa ametumwa kuwaeleza mabadiliko yamefanyika na hakuna mtu mwenye ubavu wa kuwazuia kwenda kupigakura.
Amesisitiza kuwa maandalizi ya uchaguzi huanzia kwa wapiga kura kuwa na vitambulisho vya mpigakura, akitaka wavitunze vizuri hadi wakati utakapofika wa kuvitumia.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara Mei 22, 2025, Bariadi, mkoani Simiyu, wakati akiendelea na ziara yake ya siku saba, amewahakikishia Watanzania watawaletea wagombea safi.
“Chama Cha Mapinduzi kimenituma kuwaeleza Watanzania mabadiliko yamefanyika. Msiwe na hofu yoyote, hakuna mtu mwenye ubavu wa kuwazuia kwenda kupigakura, tuendelee kuhubiri amani, nimefurahi kauli ya Mkuu wa Mkoa kwamba, Simiyu itakuwa salama, tutofautiane kwa itikani tuiache Tanzania ikiendelea kuwa na amani.
“Kama mna vitambulisho vitunzeni uchaguzi katika nchi yetu uko kila baada ya miaka mitano na ili ushike dola shinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa, pili, shida udiwani, shinda ubunge na shinda urais.
“Uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa sheria za nchi, kila Mtanzania hahitaji shahada, wanajua kila baada ya miaka mitano diwani, mbunge na Rais lazima wachaguliwe,
ndio maana mlikataa mikutano yao ya ‘No Reforms No Election’, haya maneno yao ni sawasawa na ya kwenye kanga,” amesema.
Makalla amesisitiza uchaguzi hauwezi kuahirishwa au kusogezwa mbele, hufanyika hivyo endapo kuna vita.
“Ili kuonesha kuna amani Tanzania walikuja hapa na wakawaomba na mchango. Niwakumbushe Watanzania baada ya vita ya Kagera tulitakiwa kuwa na Uchaguzi Mkuu, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akashauriwa tumetoka kwenye vita kwa nini uchaguzi usiahirishwe? Akasema ‘chama changu kinaheshimu katiba hivyo uchaguzi utafanyika’,”amesema.
Makalla amewaeleza wapinzani waliofanya mkutano wao Bariadi na kukosa wananchi, wasimlaumu Mkuu wa Mkoa, kwani hiyo si kazi yake kupeleka watu.
“Wananchi wamejenga imani kwa CCM kwa sababu wanaona huduma za kijamii zilizofanyika chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Mtu hajawahi kulima pamba anatoka Arusha anakuja Simiyu anasema nyie ni maskini, wana -Simiyu si maskini ni wachapakazi, Rais Samia ameweka alama kila kijiji, kila kata kuna huduma za kijamii za elimu, afya na barabara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED