Mtaalamu ataja mbinu kukabiliana na udukuzi

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 04:19 PM May 23 2025
Mtaalam wa masuala ya Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Mtandao, Yusuph Kileo
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Mtaalam wa masuala ya Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Mtandao, Yusuph Kileo

MTAALAM wa masuala ya Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Mtandao, Yusuph Kileo, ametoa mbinu ya kupambana na udukuzi wa mawasiliano ya simu na mitandao mbalimbali ya mawasiliano.

Miongoni mwa mbinu hizo ni pamoja na kuweka ulinzi kwa kutumia nywila ambayo si rahisi kutambuliwa kirahisi na mtu mwingine, kuacha kubonyesha ‘link’ zinazotumwa mitandaoni na kuwa na alama maalum za kuingia kwenye mitandao yako binafsi ambayo itasaidia kulinda isiingiliwe na mtu yeyote.

Kadhalika, alisema jambo la kwanza na haraka la kufanya unapogundua kwamba umedukuliwa ni kubadilisha nywila. “Kuhusu kujilinda kwenye mitandao, ni kweli kumekuwa na changamoto ya watu kuhakiwa, sisi tunashauri kwamba kama unavyoweka ulinzi kwenye mambo mengine ya kawaida, basi hata kwenye mitandao au mawasiliano yako unatakiwa kufanya hivyo,”alisema Kileo.

Mtaalamu huyo mbobezi, alitoa elimu hiyo jana kwenye warsha ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya kuelekea kwenye Mkutano wa Jukwaa la Utawala la Usimamizi wa Kimtandao Barani Afrika (AfIGF),ambalo linatarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza Tanzania kuanzia Mei 29 hadi 31 mwaka huu.

 “Huu ni mkutano mahsusi ambao kwa nchi yetu tuna bahati kubwa kwa sababu limetokea kwa mara ya kwanza, halijawahi kufanyika nchini, na limefanyika kwa sababu tumeonekana tunafanya vizuri katika eneo hilo, huu ni mkutano wa kila mtu, kuja kujadili matumizi ya mtandao,”alisema kileo.

 Alisema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni suala la usalama wa mitandao, kuongeza ushirikiano kwa nchi hizo katika eneo hilo, kuboresha miundombinu, teknolojia zinazoibukia na yale yanayohakikisha kila mmoja anapata mtandao.

 Leo Magomba ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alisema katika mkutano huo, miongoni mwa mambo makubwa mengine yatakayojadiliwa ni kuhusu matumizi ya Akili Unde.

“Tutaangalia pia masuala ya Akili Unde, tunafahamu ni teknolojia ya msingi ambayo inawezesha utendaji kazi hususani katika kipindi hiki cha mapinduzi ya nne, tano na sita ya viwanda, tunahitaji sana teknolojia hii ili kuhakikisha kwamba kazi zetu au shughuli zetu zinafanyika kwa weledi, haraka na makini katika kufanikisha masuala yote ya kijamii na kiuchumi.”

“Kwa mfano kwenye utendaji wa kazi zetu za kila siku, wito wangu ni kuwaomba Watanzania waje kwenye mkutano huu wajifunze teknolojia hii mpya kwa sababu kutakuwa na maonyesho ya mambo hayo, tunaamini watu wakijifunza vizuri kuhusu Akili Unde, tutapata wabunifu wengine,”alisema Magomba.

Dk.Nazar Kirama ni Mratibu wa Kitaifa wa Jukwaa la Usimamizi wa Intaneti kwa upande wa Tanzania, alisema zaidi ya watu 1000 kutoka nchi za Bara la Afrika na wengine kutoka nchi 10 za Ulaya wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo.

 
Dk.Kirama alisema katika mkutano huo, pia watashiriki vijana kutoka sehemu mbalimbali za Afrika na kwamba mada nyingine muhimu zitakazojadiliwa ni sera za nchi hizo zinazohusiana na usimamizi wa intaneti. “Huu ni mfumo wa kidunia ambao unaanzia Umoja wa Mataifa, unakuja Afrika mpaka unashuka Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,”alisema Dk.Kirama.