Mkoa wa Pwani umeanza mazungumzo na Wizara ya Uwekezaji ili kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wadogo kuwekeza na hivyo kusaidia kupunguza pengo la kiuchumi kati ya walionacho na wasio nacho.
Kauli hiyo imetolewa Mei 22 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara wa mkoa huo, ambao ulihusisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi kutoka wilaya zote za Pwani.
Kunenge amesema kuwa jitihada hizo zitasaidia kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kuinuka kiuchumi kama ambavyo wawekezaji wakubwa walivyofanikiwa, ambapo wengi wao walianza na viwanda vidogo kabla ya kukua na kuwa makampuni makubwa ya viwanda.
"Lengo letu ni kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kufikia hatua ya uwekezaji mkubwa. Tunahitaji kuwa na mfumo unaowaunganisha na fursa zilizopo serikalini ili nao wanufaike," alisema Kunenge.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wawekezaji kuwekeza katika maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji, akisisitiza kuwa maeneo hayo ni rahisi kuyapata, hayana migogoro, na yanasaidia serikali katika mipango ya uendelezaji wa miundombinu.
“Wawekezaji wanapowekeza katika maeneo rasmi, serikali huwa na uwezo wa kupeleka huduma muhimu kama maji, umeme na barabara kwa urahisi. Lakini hali ni tofauti pale kila mtu anaponunua eneo lake binafsi na kutarajia huduma hizo,” alieleza Kunenge.
Ameonya kuwa tabia ya baadhi ya wawekezaji kuepuka maeneo rasmi kwa kigezo cha gharama ni hatari kwa ustawi wa mpango wa kitaifa wa uwekezaji wa kimkakati.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Wafanyabiashara Taifa, Dk. Goodwill Wanga, amewataka viongozi wa wilaya kutoa takwimu sahihi kuhusu viwanda vilivyopo katika mkoa huo ili kusaidia kuwa na taarifa zinazotegemewa katika kufanya maamuzi ya maendeleo.
“Takwimu sahihi ni msingi wa kupanga maendeleo. Bila takwimu, hatuwezi kujua wapi pa kuongeza nguvu wala kupima mafanikio yetu,” alisema Dk. Wanga.
Naye Afisa Biashara wa Mkoa wa Pwani, Rehema Akida, amesema ofisi yake itaendelea kushiriki katika mabaraza ya biashara ili kuboresha mahusiano kati ya sekta binafsi na serikali, pamoja na kuchochea maendeleo ya uchumi wa mkoa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED