Mchinjita asimulia mshikemshike na askari kituo cha mwendokasi

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 06:12 PM May 23 2025
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita.
Picha:Mtandao
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, ameeleza kutoridhishwa na kitendo cha kuzuiwa na wafanyakazi wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) alipokuwa akizungumza na abiria katika Kituo cha Mwendokasi Kimara, hali iliyopelekea kushikiliwa na Polisi kwa zaidi ya saa tano.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuachiwa katika Kituo cha Polisi Mbezi, Mchinjita alisema kuwa alikuwa amekwenda katika kituo hicho kama abiria wa kawaida, akafuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kukata tiketi, lakini alizuiwa kuzungumza na wananchi waliokuwa wakisubiri usafiri.

“Nilifika kama abiria wa kawaida, nikiwa na nia ya kuzungumza na wananchi kupata uzoefu kuhusu huduma. Cha kushangaza, wafanyakazi wa Udart walinijia na kunizuia kwa madai kuwa nahitaji kibali maalumu kuzungumza na abiria,” amesema Mchinjita.

Ameeleza kuwa hali hiyo ilisababisha mzozo, ambapo wafanyakazi hao walitoa taarifa kwa polisi ambao walifika na kujaribu kumkamata kwa nguvu, huku wakivunja baadhi ya vitu vyake vya kibinafsi ikiwemo simu na kuwalazimisha waandishi wa habari waliokuwa naye kufuta picha na video walizorekodi.

“Polisi walitufikisha Kituo cha Polisi Mbezi, ambako tulishikiliwa kwa muda mrefu bila maelezo ya wazi. Tulielezwa tu kuwa Udart walikuwa na taarifa kutoka serikalini kuwa mabasi mengine yalikuwa njiani, jambo ambalo halikuwa na msingi wakati wananchi walikuwa wamekaa kwa saa kadhaa bila huduma,” amesema.

Mchinjita ameongeza kuwa hali aliyoikuta Kimara ni ya kusikitisha, ambapo wananchi walikuwa wakisubiri mabasi kwa muda mrefu huku hakuna taarifa wala usaidizi wowote wa haraka.

“Hali ya usafiri wa mwendokasi ni tete, kuna upungufu mkubwa wa mabasi kama ambavyo ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilieleza. Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kuongeza magari au kutoa fursa kwa waendeshaji wa ndani kusaidia kupunguza mzigo,” amesema.

Ameongeza kuwa baadhi ya watu walipewa dhamana ya kusimamia mradi wa mabasi hayo lakini wamefeli, na sasa hali ni mbaya kiasi cha kuhatarisha maisha ya wananchi.

“Watu wanakanyagana, wanavunjika miguu, kuna msongamano mkubwa, na nusu ya magari hayafanyi kazi. Inaonekana kuna mambo ya kifisadi yanafichwa kwenye uendeshaji wa mradi huu,” ameongeza Mchinjita.

Alipoulizwa kama polisi waliwafungulia kesi, Mchinjita amesema hawakufunguliwa mashitaka yoyote, na waliambiwa kuwa watapewa wito iwapo watatakiwa kufika tena kituoni.