Zaidi ya washiriki 1,200 kutoka mataifa mbalimbali duniani wanatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam, Tanzania, kushiriki katika Mkutano wa Jukwaa la Utawala wa Mtandao Afrika (AfIGF) utakaofanyika kuanzia Mei 29 hadi 31, mwaka huu, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mhandisi wa Miundombinu ya Mawasiliano kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Leo Magomba, alisema mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu kwa wadau kujadili masuala nyeti yanayohusu maendeleo ya intaneti na teknolojia barani Afrika.
“Mkutano huu ni muhimu sana kwa sababu, kwa mujibu wa takwimu za ITU za mwaka 2024, ni asilimia 38 pekee ya Waafrika wanaotumia intaneti ya uhakika, na kwa dunia nzima ni asilimia 68. Hii inaonyesha pengo kubwa,” alisema Magomba.
Alisema kuwa mkutano huo utatoa fursa kwa wadau kutoka sekta mbalimbali kujadiliana kuhusu njia za kuongeza upatikanaji wa intaneti kwa wote, kuondoa tofauti ya matumizi kati ya mijini na vijijini, pamoja na kuimarisha usalama wa mtandao.
Kadhalika, teknolojia ya Akili Bandia (AI) itapewa kipaumbele, ikizingatiwa mchango wake mkubwa katika kurahisisha kazi na kuongeza ufanisi, hususan katika zama za nne na tano za Mapinduzi ya Viwanda.
“Tunahitaji kuangalia namna bora ya kutumia teknolojia hii kwa maendeleo ya Afrika,” alisema Magomba.
Mkutano huo pia utajadili mahusiano ya kimataifa katika usimamizi wa mtandao, kwa kuzingatia kuwa suala hilo linahitaji ushirikiano wa mataifa yote na si la nchi moja pekee.
Tanzania inatarajia kunufaika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu, kwa kuimarisha nafasi yake katika majukwaa ya kimataifa ya TEHAMA, pamoja na kupata ujuzi, mitazamo na ushirikiano mpya wa kimkakati kutoka kwa wadau wa kimataifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED