Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga imeendesha mafunzo kwa waandishi wa habari mkoani hapa, yakiwa na lengo la kuwaongezea uelewa na weledi katika kuripoti habari za kimahakama kwa usahihi na kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo.
Mafunzo hayo yamefanyika leo Mei 23, 2025, katika ukumbi wa Mahakama Kuu ambayo yamefunguliwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Seif Kulita.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Jaji Kulita amesema hatua hiyo imekuja baada ya waandishi wa habari kuwasilisha ombi lao katika kikao cha tathmini ya Siku ya Sheria nchini kilichofanyika Februari 6, mwaka huu, wakitaka kujengewa uwezo wa kuripoti masuala ya Mahakama kwa usahihi na weledi zaidi.
“Mafunzo haya yatawawezesha kuelewa vyema muundo wa Mahakama, matumizi ya TEHAMA katika usikilizaji wa mashauri kwa njia ya kidijitali, pamoja na namna bora ya kuripoti habari za kimahakama kwa kuzingatia maadili ya uandishi,” amesema Jaji Kulita.
Aidha, amesema kuwa kwa sasa Mahakama inazidi kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa haki, hivyo ni muhimu waandishi wa habari wakawa na uelewa sahihi kuhusu mabadiliko hayo.
Baadhi ya waandishi walioshiriki mafunzo hayo akiwamo Sayi Mathias,wamesema kuwa yamekuwa chachu ya kuongeza maarifa na uelewa kuhusu taratibu za kimahakama, hatua ambayo itawasaidia kuripoti kwa usahihi habari za Mahakama bil kuingilia uhuru wa Mahakama.
“Tunaishukuru Mahakama kwa kutusikiliza na kutupatia mafunzo haya. Tumejifunza mengi, hasa kuhusu jinsi ya kutumia lugha sahihi tunaporipoti kesi au maamuzi ya Mahakama,” amesema Sayi.
Mahakama ya Tanzania imekuwa ikiendelea na jitihada mbalimbali za kushirikiana na wadau wake, ikiwamo vyombo vya habari, katika kuhakikisha upatikanaji wa haki unakuwa wa wazi na unaoeleweka kwa wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED