Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura amewavisha vyeo Askari Polisi 208 ngazi ya Koplo, Sajenti na Sajini Meja wa Polisi.
Kamanda Kuzaga amewavisha vyeo Mei 23,2025 na kuwataka Askari hao kudumisha nidhamu katika utekelezaji wa kazi zao za kila siku na kuleta mabadiliko chanya ndani ya Jeshi la Polisi.
“Jeshi la Polisi linatambua mchango wa kila Askari na litaendelea na utaratibu wake wa kupandisha vyeo na kutoa zawadi mbalimbali kwa Askari kutoka na utendaji unaozingatia nidhamu, haki, weledi na uadilifu,”alisema Kamanda Kuzaga.
Mmoja wa Askari aliyevishwa cheo Sajini Meja wa Polisi Benson Lucka wa Polisi Wilaya ya Mbeya amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura kwa kuwapendekeza na kuwapandisha vyeo kutokana na utendaji kazi wao.
Askari hao wamevishwa vyeo baada ya kupendekezwa na kisha kuhudhuria na kuhitimu mafunzo ya uongozi mdogo katika vyuo na Shule ya Polisi Tanzania (TPS) zamani ikijulikana CCP iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED