Wenye fistula wanaotelekezwa na wenza zao wakumbwa na sonona

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 06:06 PM May 23 2025
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera

Wanawake wanaokumbwa na tatizo la Fistula nchini wanadaiwa kutelekezwa na wenza wao, hali inayowasababishia msongo wa mawazo (sonona) na kuwafanya washindwe kujitokeza kupata matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, alipomwakilisha Waziri wa Afya katika maadhimisho ya Siku ya Fistula Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Hospitali ya Kanda ya Rufani Mbeya, kitengo cha wazazi Meta.

Homera amewataka wanaume kuacha kuwatelekeza wake zao pindi wanapopatwa na changamoto hiyo au matatizo mengine ya kiafya, na badala yake wawapeleke hospitalini kwa ajili ya kupata huduma.

“Wataalamu wamesema Fistula inatibika na mama anarudi katika hali yake ya kawaida. Kwa hiyo, nawasihi wanaume kuonyesha upendo wa kweli kwa wake zao kama tulivyoapa kuwa pamoja katika shida na raha,” amesema Homera.

Aidha, ametoa wito kwa jamii kuacha unyanyapaa dhidi ya wanawake wenye fistula na badala yake kuwahamasisha kwenda kupata matibabu, akisisitiza kuwa huduma hizo zinatolewa bure.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Fistula Tanzania, Clement Ndahani, amesema matibabu ya tatizo hilo ni ya gharama kubwa, jambo ambalo linawafanya wanawake wengi kushindwa kuyamudu.

Ameeleza kuwa taasisi yake imekuwa ikishirikiana na hospitali za kanda kutoa huduma za matibabu kwa wanawake hao, ikiwa ni pamoja na kuwaibua, kuwasafirisha, kugharamia matibabu yao, na kuwajengea uwezo madaktari bingwa wa upasuaji wa fistula.

“Fistula inasababisha wanawake kukosa kujiamini, kushindwa kuchangamana na wenzao, na hata kuathiri shughuli zao za kiuchumi. Tunawasaidia sio tu kupata matibabu, bali pia kupona kisaikolojia ili warudi kwenye maisha ya kawaida,” amesema Ndahani.

Ndahani ameongeza kuwa katika maadhimisho hayo, wanawake 15 walitibiwa ndani ya siku mbili na huduma hizo zitaendelea kutolewa katika hospitali mbalimbali nchini.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Ulimbakisye Macdonald, amewashukuru wadau kwa kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya tatizo hilo, na kueleza kuwa serikali imelenga kulimaliza kabisa ifikapo mwaka 2030.

“Kila mwaka wanabainika wanawake kati ya 2,000 hadi 3,000 wenye tatizo la fistula, lakini wanaotibiwa ni takribani 1,500 tu kutokana na sababu kama aibu na gharama za matibabu,” amesema Macdonald.