Lissu achaguliwa IDU licha ya kuwa gerezani

By Enock Charles , Nipashe
Published at 02:04 PM May 24 2025
Tundu Lissu
PICHA: MTANDAO
Tundu Lissu

Muungano wa Vyama vya kidemokraisa Duniani (IDU) umemchagua Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Tundu Lissu kuwa sehemu ya jopo la Makamu Wenyeviti wa Umoja huo.


Katika taarifa iliyotolewa na CHADEMA leo, imesema Lissu amechaguliwa kutokana na rekodi yake ya kuwa na msimamo usioyumba katika kupigania haki, utawala bora, na demokrasia nchini.

“Wajumbe wa mkutano wa IDU walitanabaisha kuwa kwa uzoefu wake katika mapambano ya kutafuta demokrasia ya kweli, haki na uhuru wa kweli, Mh Lissu atatoa mchango mkubwa” imesema sehemu ya barua hiyo.

Kesi ya uhaini na ya kuchapisha taarifa za uongo zinazomkabili Tundu Lissu, ambazo zimesikilizwa katika mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam siku ya Jumatatu, zimegonga vichwa habari kitaifa na kimataifa.

Uhaini ni kesi ambayo ukipatikana na hatia hukumu yake inaweza kuhusisha kunyongwa hadi kufa, na kesi ya kuchapisha taarifa za uongo, inaweza kukuingiza katika faini au kufungwa gerezani si chini ya miaka mitatu ama yote mawili.