KADI nyekundu ya Yusuph Kagoma mapema kipindi cha pili iliwagharimu Simba na kujikuta ikicheza pungufu muda wa mrefu wa kipindi cha pili na kulazimishwa sare ya bao 1-1 na RS Berkane.
Bao la dakika za mwisho la Soumaila Sidibe liliihakikishia Berkane ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-1 baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita nchini Morocco.
Simba jana ilianza mchezo huo kwa kasi ikilishambulia lango la RS Berkane na dakika ya tatu ya mchezo Simba walipata faulo baada ya Steven Mukwala kuchezewa vibaya lakini mpira wa Jean Ahoua ulitoka nje. Dakika ya Saba Simba walikaribia kupata bao kupitia kwa Mukwala lakini mpira wake uliokolewa na mabeki na kuwa kona tasa.
Joshua Mutale ambaye alianza kikosi cha kwanza, aliipatia Simba bao la kuongoza baada ya kuuwahi mpira wa krosi uliopigwa na Elie Mpanzu na kuachia shuti lilojaa nyavuni. Baada ya goli hilo, Simba waliendelea kuliandama lango la Berkane na dakika ya 23, Kapombe alikosa goli baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Mutale lakini mpira huo ulidunda chini na kutoka nje.
Berkane walijibu mapigo dakika ya 37 baada ya mpira wa tikitaka wa Hamza El Moussaoui kupanguliwa na kipa Moussa Camara na kuwa kona ambayo hata hivyo haikuza bao. Mpaka dakika 45 zinamalizika Simba walienda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili Simba walikianza kwa kasi kujaribu kusaka bao la pili, hata hivyo walipata pigo mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kiungo Yusuph Kagoma kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea rafu kiungo wa Berkane.
Kadi hiyo ilionekana kuwavuruga Simba na kuwaamsha Berkane ambao walianza kumiliki mpira na kupanga mashambulizi. Kocha wa Simba, David Fadlu, alifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kumtoa Mutale na nafasi yake kuchukuliwa na kibu Denis, na baadae kuwatoa Mohamed Hussein nafasi yake kuchukuliwa na Valentin Nouma.
Dakika ya 53, Mukwala akiwa ndani ya boksi aliikosesha Simba bao baada ya shuti lake kupaa juu ya lango la Berkane. Simba walipata bao dakika ya 72, lakini mfungaji, Mukwala alikuwa ameotea.Zikiwa tayari zimeonyeshwa dakika tisa za kufidia muda uliopotea, Sidibe aliisawazishia Berkane baada ya mqbeki wa Simba kujichanganya kuondoa mpira golini kwao, ambapo ulimkuta mfungaji aliyeachia shuti la chini chini lililomshinda Camara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED