WACHIMBAJI wadogo wa mgodi wa Isanjabadugu uliopo kata ya Nyakafulu Halmashauri ya Mbogwe mkoani Geita, wameweza kulipa mrahaba wa serikali zaidi ya Sh.bilioni 3.663, baada ya kupata nishati ya umeme wa uhakika na kuwaondolea gharama kubwa za uendeshaji tangu mwaka 2020.
Katibu wa Mgodi huo, Patrick Basoga ameyabainisha hayo leo wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari vilivyofika mgodini kujua namna wachimbaji walivyoweza kunufaika na uwepo wa rasilimali hiyo ikiwemo kulipa mirahaba ya serikali pasi kuvutana na mamlaka husika.
Amesema, tangu wamepata umeme mwaka 2020 maduhuri pia yameongezeka na wameweza kukusanya mapato ya serikali Sh.bilioni 3.673 kati yake mrahaba ilikuwa Sh.bilioni 1.925, ushuru wa halmashauri Sh.bilioni 1.59 huku ushuru wa huduma ikiwa ni kiasi cha Sh.milioni 679.
Basoga amesema, mafanikio haya yanatokana na kupunguziwa gharama za uendeshaji na serikali baada ya kupata nishati hiyo, kwani tangu mwaka 2017 mgodi ulipoanza uzalishaji kwa mara ya kwanza walikuwa watumia majenereta kwenye uchimbaji wao na kwa siku walitumia mafuta lita 500 mpaka 1000.
"Tunaipongeza serikali kwa kutusikiliza na kututatulia changamoto yetu ya umeme migodini na sasa tunauwezo wa kulipa maduhuri ya serikali na wenyewe tukanufaika na rasilimali hii: Ombi letu kile kinachopatikana kirudi kwetu kurekebisha miundombinu ya barabara ili tupate urahisi wa kupitisha madini mpaka sokoni" Ameongeza.
Nae Meneja wa Mahina Gold Mine, Frank Joseph amesema, kwa kipindi cha uongozi wa miaka minne ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wamenufaika na uwepo wa rasilimali hiyo kwa kujiinua kiuchumi, kusogezewa masoko karibu pamoja na kulipa mapato yake kwani mpaka sasa wameshalipa zaidi ya Sh.milioni 700.
Amesema, gharama za uendeshaji wa shughuli za uchimbaji madini ni kubwa kulinganisha na kile wanachokipata na endapo serikali kupitia Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati wasingewapatia umeme, wengi wao wangekuwa wamashafirisika na kufungwa na taasisi za kifedha kwa kushindwa kulipa mikopo waliyochukua kuendesha shughuli zao.
Aidha Joseph ameomba serikali kuboresha upatikanaji wa umeme mgodini kwani unawafikia kwa single phase na kukatika mara kwa mara kwani wanahofia mashine zao kuungua na kushindwa kuendelea kufanya uzalishaji, kulipa kodi na kujiingizia kipato cha familia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED