Rais wa zamani wa DRC Joseph Kabila amewataka wananchi kupambana na udikteta

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:41 AM May 25 2025
Rais wa zamani wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) Joseph Kabila
PICHA: MTANDAO
Rais wa zamani wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) Joseph Kabila

Rais wa zamani wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) Joseph Kabila amewataka wananchi kupambana na kile alichokiita udikteta huku akimlaumu mrithi wake Rais Felix Tschisekedi kwa kuiingiza nchi katika machafuko.

Pia ametoa wito kwa wananchi kuungana ili kurejesha utawala wa sheria na utulivu, akielekeza lawama kwenye mfumo wa haki wa nchi hiyo baada ya baraza la seneti kupiga kura ya kuondoa kinga yake, na kumfungulia njia ya kushtakiwa kwa madai ya uhaini na uhalifu wa kivita.

Kabila ameyasema hayo kupitia video ya moja kwa moja iliyosambaa kwenye mtandao kutoka eneo lisilojulikana, siku moja baada ya kupoteza kinga yake kwa madai ya uhusiano na kundi la M23.

"Mfumo wa haki umekuwa chombo cha ukandamizaji kwa udikteta unaojaribu sana kuendelea kuwa mamlakani," amesema.

Kabila ambaye anakanusha kuwaunga mkono waasi wa M23 ambao wameiteka miji miwili mikubwa mashariki mwa nchi hiyo iliyokumbwa na mizozo, amekuwa uhamishoni tangu 2023.

Rais huyo wa zamani, ambaye amesema mara kwa mara kuwa anarejea kutoka uhamishoni kusaidia kupata suluhisho la mgogoro huo, aliishutumu Kinshasa kwa kuchukua maamuzi ya kuudhi kwa mzaha.

“Nimeamua kuvunja ukimya, kwa sababu kwa kuzingatia hali ambayo nchi yetu inapitia, kuendelea kukaa kimya kungenifanya nifunguliwe mashtaka mbele ya mahakama ya historia, kwa kushindwa kusaidia zaidi ya watu milioni mia moja walio hatarini”, amasema Kabila.

Kabila amesema uhuru wa DRC na uadilifu wa eneo hauwezi kujadiliwa, akisema kama mwanajeshi, aliapa kutetea nchi yake... Ninabaki kuwa mwaminifu zaidi kuliko hapo awali kwa kiapo hiki," alisema.