Wakili wa Tundu Lissu, Peter Kibatala amelalamikia kunyimwa fursa ya kuonana na mteja wake kwa faragha na kuomba mteja wao huyo kutendewa haki.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Wakili Kibatala amesema pamoja na kwamba Lissu anashitakiwa kwa kosa la uhaini ambalo halina dhamana lakini ni haki yake kisheria kupewa faragha kuonana na mawakili wake tofauti na alivyodai Kibatala kwamba fursa hiyo ni ndogo kwao.
“Misingi ya kawaida ya kuhudumia wafungwa iliyopitishwa na Baraza la Umoja wa Taifa inasema wafungwa wote watapewa nafasi ya kuwasiliana na mawakili au wasaidizi wao wa kisheria bila kuchelewa, magereza wana haki ya kushuhudia kinachotendeka lakini sio kusikiliza tunachoongea na mteja wetu” amesema Kibatala.
Lissu alikamatwa na polisi wilayani Mbinga mkoani Ruvuma muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa hadhara mapema mwezi Aprili na baadae kusafirishwa hadi Jijini Dar es Salaam na kufunguliwa mashtaka mawili ikiwemo la uhaini lisilo na dhamana jambo lililomfanya kukaa gerezani hadi leo akisubiri mwendelezo wa kesi yake.
Lissu na chama chake wapo katika kampeni ya kupigania kile wanachodai ni mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi waliyoipa jina la "no reforms no election" ambapo mpaka sasa imeshafanyika katika mikoa ya kanda ya kusini na katika mkoa wa Dar es Salaam.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED