Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga, unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi katika mkoa huo na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 3, 2025 na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, wakati wa ziara yake pamoja na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Shinyanga na Mwanza katika eneo la ujenzi wa uwanja huo.
Amesema ukarabati wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga, ni miongoni mwa viwanja 11 ambavyo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha za kuvikarabati ili kurahisisha usafiri na kufungua fursa za kiuchumi.
“Uwanja huu utafungua njia za mawasiliano ya anga, kurahisisha usafiri na kuleta fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wa Shinyanga na maeneo jirani,” amesema Msigwa.
Kwa upande wake, Mhandisi Jiyando Matoke kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)amesema ujenzi wa uwanja huo ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo Juni 10, 2025 kwa gharama ya Shilingi bilioni 44.8.
Amesema kuwa ujenzi huo umefikia asilimia 80, huku uwanja huo ukiwa tayari umeanza kupokea ndege za dharura zinazoweza kutua na kuruka. Aidha,amesema kuhusu ulipaji wa fidia, kwamba wameshalipa Sh.milioni 764 kwa wananchi waliopisha ujenzi huo.
Kwa upande wa ajira amesema ujenzi huo umeajiri watu 240, ambapo kati ya hizo, ajira 230 ni kwa wazawa na asilimia tano raia wa kigeni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED