Madiwani Msalala wagawanyika baada ya mbunge kujadiliwa kwenye baraza

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 04:22 PM May 02 2025
Madiwani wanne kati ya 23 wa Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, wakizungumza na vyombo vya habari juu ya hoja ya kumpeleka mbunge wao Iddi Kasimu kwenye kamati ya maadili ya madiwani leo.
Picha: Shabani Njia
Madiwani wanne kati ya 23 wa Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, wakizungumza na vyombo vya habari juu ya hoja ya kumpeleka mbunge wao Iddi Kasimu kwenye kamati ya maadili ya madiwani leo.

Madiwani wa Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga wamegawanyika katika makundi mawili kuhusu msimamo wa kumfikisha Mbunge wao, Iddi Kasimu, mbele ya Kamati ya Maadili ya Madiwani kwa madai ya kuwadhalilisha kwenye mikutano ya hadhara.

Mgawanyiko huo ulijitokeza kufuatia kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Aprili 30, 2025, ambapo baadhi ya madiwani waliibua hoja ya Mbunge huyo kuwadhalilisha hadharani, kutohudhuria vikao vya baraza mara kadhaa, na hivyo kuomba ahojiwe na Kamati ya Maadili ya Baraza.

Hata hivyo, baadhi ya madiwani wamepinga hoja hiyo wakidai kuwa kikao hicho kilikiuka taratibu na miongozo ya uendeshaji wa vikao vya halmashauri kwa kuingiza ajenda isiyoidhinishwa katika kikao cha ndani cha chama (Kokasi), ambapo ajenda rasmi hupangwa kabla ya kuwasilishwa kwenye kikao cha baraza.

Diwani wa Kata ya Busangi, Alexander Mihayo, amekosoa hoja hiyo akisema kuwa hakuna makubaliano ya pamoja yaliyofikiwa kwenye kikao cha Aprili 30 kuhusu kumfikisha Mbunge mbele ya Kamati ya Maadili. Alisema waliompinga Mbunge ni baadhi ya madiwani ambao hushindwa kutoa majibu ya miradi mbele ya wananchi na hivyo kuhisi kudhalilishwa.

“Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, madiwani wengi wamejaa joto la kisiasa. Mbunge akitusimamisha mbele ya wananchi kuulizwa kuhusu miradi, na hatuna majibu, tunahisi kudhalilishwa. Lakini huo ni wajibu wetu kama wawakilishi wa wananchi,” amesema Mihayo.

Naye Diwani wa Viti Maalum Kata ya Isaka, Pily Izengo, amesema amekuwa akiambatana na Mbunge kwenye ziara zake za kusikiliza changamoto za wananchi na hajawahi kushuhudia wala kusikia Mbunge huyo akiwadhalilisha madiwani mbele ya wananchi.

Amesema pia ni mjumbe wa Mfuko wa Jimbo, na kwamba fedha hugawiwa kulingana na mahitaji ya kata mbalimbali huku miradi ya kipaumbele ikiibuliwa na wananchi. Alisema kiasi cha Sh milioni 79 kimepokelewa kwa utekelezaji wa miradi kadhaa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ngaya, Kisusi Ilindilo, amesema kuwa mwaka 2021 kata yake haikuwa na umeme, lakini kutokana na juhudi za Mbunge, vijiji vyote, vitongoji viwili na kituo cha afya vimeunganishwa na nishati hiyo, hali iliyopunguza adha kwa wajawazito waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma za uzazi.

Diwani wa Kata ya Mwalungulu na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Frola Sagasaga, amesisitiza kuwa kikao cha Aprili 30 hakikufuata utaratibu wa kikanuni, kwa kuwa ajenda ya kumjadili Mbunge haikuwamo katika orodha rasmi ya ajenda zilizotolewa.

Amesema kuwa kama kweli kulikuwa na haja ya kujadili suala hilo, ilipaswa kuanzia kwenye kikao cha chama (Kokasi) ambako kunapangwa ajenda za baraza kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya kikanuni.

“Hata mimi niliwahi kuulizwa hadharani kuhusu miradi ya maendeleo, lakini kwa kuwa nilikuwa na majibu ya kutosha, sikuona kama ni kudhalilishwa. Ni wajibu wetu kuwajibika mbele ya wananchi,” amesema Sagasaga.